MSD yafanya maboresho makubwa sekta ya afya Singida, yatoa vifaa tiba, dawa


Na Mwandishi Wetu, Jamhurimedia, Singida
BOHARI ya Dawa (MSD) imetoa vifaa tiba na dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 532.4 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Hospitali ya Wilaya ya Singida, Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Hosptali ya Wilaya ya Ikungi na Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu mkoani hapa.

Akizungumza Oktoba 12, 2023 wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwenye hospitali hizo, Meneja wa MSD Kanda ya kati Dodoma, Mwanashehe Jumaa alivitaja vifaa tiba na dawa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kuwa ni vitanda 9 (ICU Beds) vya kisasa pamoja na dawa.

Amesema kwa Hospitali ya Wilaya ya Singida vifaa vilivyotolewa ni vitanda viwili vya kisasa vya umeme (ICU Beds), wakati kwa Kituo cha Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kikipokea pasi kubwa ya kunyoshea nguo ( Flat iron industry), vitanda vya wagonjwa, vitanda vya kujifungulia, mashuka, magodoro na viti mwendo.

Mwanashehe alisema utoaji wa vifaa hivyo ni muendelezo wa uboreshaji wa huduma za sekta ya afya mkoani Singida kwani Machi 15, 2023 MSD ilitoa mashine za kufulia, vifaa vya kinywa na meno, usingizi na vitanda Hosptali ya Wilaya ya Singida Ilongero.

Baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Wataalam kutoka MSD walitoa maelekezo na mafunzo kwa wataalam ambao hospitali zao zimenufaika na vifaa hivyo, ili wavitunze na vidumu muda mrefu kwani Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua.

“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kununua vifaa hivi, hivyo ni wajibu wa watumishi wa sekta ya afya kuhakikisha vinatunzwa vizuri,” alisema .Mfamasia wa Kanda hiyo na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna.

Viongozi wa Hospitali hizo wameishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuendelea kuwapatia dawa na vifaa tiba kwa wakati jambo ambalo limeongeza tija na ufanisi wa kazi katika utoaji huduma za afya.

Nao Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Paul Ndeki, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Singida, Yusuph Kitinya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itigi, Emmanuel Mallange, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hussein Sapoko waliahidi kuvitunza na kumshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuboresha huduma za afya mkoani humo.

“Vifaa tulivyopatiwa vitatusaidia kutoa huduma zetu tunawashukuru Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa vifaa tiba kupitia MSD hivyo kuhimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.,.” alisema Kitinya.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli alisema wamepokea vitanda 16 na kufikisha idadi ya vitanda 80 na kueleza kuwa mbali ya vifaa hivyo pia walipokea baadhi ya vifaa vingine vingi kama magodoro, mashuka, taa za kufanyia uchunguzi, taa ya chumba cha upasuaji na sasa wapo kwenye mchakato wa kupelekewa mashine itakayosaidia kufanya operesheni ya mama na mtoto katika jengo ambalo lipo mbioni kukamilika.

.”Kwa ujumla ni idadi kubwa ya vifaa tulivyoletewa na Serikali chini ya mama yetu kipenzi Rais Samia kupitia MSD.” alisema Dk.Kimotoli.

Kwa upande wake Mganga wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Hussein Sepoko alisema Rais Samia amewapelekea vifaa tiba vingi vya kisasa na akaishukuru MSD kwa ushirikiano inayowapa wa kuwapelekea vifaa tiba na dawa kwa wakati.

Nao Diwani wa Kata ya Ilongero Issa Mwiru na Diwani wa Kata ya Itigi Mjini, Ally Minja walipongeza Serikali na MSD kwa kusambaza vifaa tiba na dawa.

“Kwa nafasi ya kipekee tunaishukuru MSD wamekuwa na ushirikiano mkubwa tunapohitaji vifaa tiba na dawa wanatuletea kwa wakati hakika wameendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya ,” alisema Mwiru.

Aidha, Mwiru aliishukuru Serikali kwa kuwaletea watumishi katika hospitali mpya ya Wilaya ya Singida na kusifia utendaji kazi wao kwa masaa yote wanapokuwa kazini.