Na Benny Kingson,JamhuriMedia,Tabora

Salma Hamis Maulid (34), mkazi wa Mtaa wa Mbirani, kata ya Kidongo-Chekundu katika Halmashauri ya Manispaa Tabora ameuawa na mume wake na kisha kuzikwa chumbani.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo na kuongeza kuwa baada ya kuuawa, muuaji alimzika chumbani na kusakafia vizuri ili watu wasijue.

Amesema tukio hilo limetokea Machi 7, mwaka huu, katika mtaa huo ambapo Michael Hendry mkazi wa Mbirani ambaye anaishi jirani na nyumba ya wanandoa hao aligundua tukio hilo baada ya kufika nyumbani hapo na kukuta ukimya

Shuhuda huyo ameeleza kuwa baada ya kuona siku kadhaa zimepita bila wanandoa hao kuonekana na chumba chao kufungwa walilazimika kuvunja mlango wa chumba hicho na kukuta sakafu ambayo haijakauka vizuri chini ya kitanda.

Amesema walipata hofu iliyopelekea kufukua eneo hilo na kukuta mwili wa mtu umezikwa kwenye shimo hilo ambapo alieleza kuwa baada ya kupata taarifa walifika eneo la tukio na kufanya uchunguzi ambapo ilibainika baada ya mwanaume huyo kufanya mauaji hayo na kuzika mwili chumbani alitokomea kusikojulikana.

Kamanda Abwao ameongeza kuwa kutokana na uchunguzi wa awali na ushuhuda wa majirani ilibainika chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi uliosababishwa na wivu wa kimapenzi waliokuwa nao wanandoa hao.

“Tunaendelea kumtafuta mtuhumiwa popote alipo ili sheria ichukue mkondo wake ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya dola, naomba wananchi hususani majirani watupe ushirikiano ili akamatwe” amesema.

Kamanda huyo ametoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa watu wanaokuwa na ugomvi nao na kuwataka kufuata taratibu ikiwemo kutumia viongozi wao wa dini ili kumaliza migogoro yao kwa amani na utulivu.