Msanii wa filamu nchini Jacob Stephan Maarufu JB ametabiri kuwa tasnia ya Bongo Movie itafanya vizuri mwaka 2018 kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa mwaka 2017.

Muigizaji huyo mwenye vituko vingi, amedai wasanii wengi wamefanya maandalizi makubwa katika kufungua kampuni za kusambaza filamu pamoja na kuzipeleka filamu kwenye majumba ya sinema.

“Mwaka 2018 itakuwa nzuri zaidi kwa Bongo Movie kwani ukiangalia kurasa zao tayari wamerudi kwenye kazi zao. Kitu ambacho tulikuwa tukitamani ni ujio wa makampuni ya usambazaji, barazani, max burudani umeongeza chachu zaidi kwani hilo lilikuwa tatizo kubwa,” ameandika JB kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Ameandika kuwa, “Lakini pia kumekuwa na utengenezaji wa tamthilia nyingi ambazo zitashindana sana mwezi January.

Uzinduzi wa filamu mbalimbali kwenye kumbi kubwa tena zikionyeshwa live kwenye TV nalo limekuwa jambo zuri.

Nawapongeza waandaji wote wanao hakikisha Bongo Movie inashika kasi mpya, hongereni.

Muigizaji huyo mwanzoni mwa mwaka 2017 alisema ifikapo mwisho wa mwaka 2018 atatangaza kustaafu kuigiza na kubaki kama producer tu lakini bado haijajulikana kama atafanya maamuzi hayo ama bado ataendelea kupambana katika game la uigizaji.

By Jamhuri