Na Tatu Saad,JamhuriMedia

Bondia kutoka Jijini Tanga, Tanzania, Hassan Mwakinyo anaendelea na maandalizi ya pambano lake dhidi ya raia kutoka DR Congo, Kuvesa Katembo mnamo April 23 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Mwakinyo amesema baada ya kukaa muda mrefu bila kucheza katika ardhi ya nyumbani huu ni wakati wake wa kuwakumbusha mashabiki zake uwepo wake.

Amesema kwa maandalizi aliyoyafanya anaamini kuwa katika pambano hilo ushindi utabaki nyumbani (Tanzani) na itakuwa ni sehemu ya kuendeleza rekodi yake ya ushindi katika ardhi ya nyumbani.

“Najua mashabiki wangu walikuwa na hamu ya kuona kile kilichotokea katika michezo iliyopita nawaahidi kuwa pambano hili litakuwa la aina yake narudi ulingoni baada ya kupoteza lakini nawaahidi watarajie mchezo mzuri siku hiyo,” amesema Mwakinyo.

Mara ya mwisho Mwakinyo kucheza pambano hapa nchini ilikuwa Septemba 3, 2021 aliposhinda kwa TKO.

Mwakinyo anatarajiwa kupanda ulingoni Aprili 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma katika pambano la raundi 10 lisilokuwa la ubingwa.

Pambano hilo limeandaliwa na Kampuni ya Lady in Red Promotion chini ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Sophia Mwakagenda, likilenga kukusanya taulo za kike kwa wanafunzi wa Nyanda za Juu Kusini.

By Jamhuri