Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na viongozi wa madereva wa pikipiki mkoani humo wamewatembelea wahanga wa ajali za pikipiki na vyombo vingine vya moto katika Hospitali ya Nkoranga Lutheran iliyopo Arumeru mkoani Arusha.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu wa Polisi SP Solomon Mwangamilo akiongozana na askari wa kikosi hicho amesema kuwa lengo la kufika katika hospitali hiyo ni kukusanya taarifa zao na kutoa pole kwa wahanga wa ajali ambapo amebainisha kuwa hospitali hiyo ni maarufu kwa kutibu magonjwa waliopata madhara yatokanayo na ajali mbalimbali.

Aidha SP Mwangamilo ameeleza kuwa wao kama Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha wameona ni vyema wafike katika hospitali hiyo ambayo inapokea wagonjwa wengi wa ajali kutoka mikoa ya kanda ya kasikazini.

Mwangamilo amesema kuwa katika msafara huo wameambatana na viongozi wa madereva wa pikipiki maarufu bodaboda katika mkoa huo ambapo lengo la kuambatana na viongozi hao ni kutokana na ajali nyingi kusababishwa na madereva wa pikipiki.

Naye katibu wa waendesha pikipiki Wilaya wa Arusha, Hakimu Msemo amebainisha kuwa wapo baadhi ya madereva pikipiki ambao wamekuwa wakiendesha vyombo hivyo kwa kukiuka sheria za usalama barabarani

Sambamba na hilo ameongeza kuwa wao watakuwa mabalozi wazuri kufikisha kile ambacho wamekiona kutokana na waliyoyaona na mfano walio uona kwa wahanga wa ajali za pikipiki.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti kwa Chama cha Waendesha Bodaboda Wilaya ya Arusha Hemed Mbaraka amesema wao kama viongozi wamejifunza nakusema kuwa wanakwenda kuwa waeleza namna ajali zinavyo waacha wananchi na madhara ya kudumu.

By Jamhuri