Na Mwandisho Wetu, JamhuriMedia, Tabora

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga kuunda timu maalum ya kufanya tathmini kwa vyuo vyake vya Ardhi Tabora na Morogoro na kushauri namna bora ya kuboresha vyuo hivyo.

‘’Wizara inakwenda kuandaa timu maalum kuja kufanya upya mapitio ya vyuo vyetu vya ardhi ikiwemo makusanyo ya ndani ili kupima uwezo wa mapato ya ndani’’ alisema Pinda

Pinda ametoa agizo hilo tarehe 8 Desemba 2023 wakati wa Mahafali ya 41 ya Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) yaliyofanyika chuoni hapo mkoani Tabora.

Ametoa siku saba kuanzia tarehe 8 Desemba 2023 kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi kuunda timu hiyo haraka itakayofanya ukaguzi wa mahesabu, makusanyo ya mapato ya ndani na kutoa ushauri pamoja na mambo mengine namna bora ya kutumia mapato ya ndani kwa ile miradi ya maendeleo.

Aidha, timu hiyo itaangalia pia suala la ajira kwa watumishi ambapo kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi vyuo hivyo vya ardhi vinatumia wastani wa Shilingi milioni 80 hadi 100 kwa walimu wa muda pekee kiasi alichokieleza ni kikubwa.

‘’Katika vyuo vyetu walimu wa muda kwa muhula wanatumia takriban Tsh milioni 80 hadi 100 kwa muhula mmoja kiasi hiki ni kikubwa tunaweza kuajiri walimu na sehemu ya watumishi wa chuo na kupunguza uhaba wa watumishi unaokabili vyuo’’ alisema Pinda.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARITA) Dkt Lucy Shule amemueleza Naibu Waziri Pinda kuwa, Chuo hicho cha Ardhi kinakabiliwa na upungufu wa watumishi, vyumba vya madarasa, Maabara pamoja na vyumba vingine vya mafunzo.

‘’Tunaiomba wizara kuongeza majengo ya maabara ya uchoraji, uchapishaji na kompyuta, hii inatokana na ukweli kuwa mojawapo ya nguzo za ubora wa mafunzo kwa vitendo ni ubora wa maabara na vifaa vimavyotumika’’ alisema Dkt Shule

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Ushauri ya ARITA, ubora wa wahitimu na mafanikio ya wanafunzi wa chuo hicho inategemea sana ubora wa program na kozi walizozisoma pamoja na mchakato wa mafunzo kwa vitendo waliyoyapitia.

Ameiomba Wizara ya Ardhi kukiongezea chuo hicho vitendea kazi vya kujifundishia alivyovieleza kuwa vitawasaidia wanafunzi kupata ujuzi na stadi zilizolengwa katika mafunzo yao na kuwawezesha kuwa na umahiri katika kufanya kazi zao kwa kujiamini na ubora unaokidhi viwango vya mahitajio ya soko.

Jumla ya wahitimu 1,132 wametunukiwa Astashahada na Stashahada katika fani za Usimamizi wa Mazingira, Mifumo ya Taarifa za Kijiofrafia, Sanaa, Ubunifu na uchapishaji, Urasimu Ramani pamoja na Usimamizi wa Ardhi, Uthamini, na usajili.