Nani mkweli kati ya GSM, Makonda?

Na Mwandishi Wetu

Mgogoro wa kugombea eneo la kiwanja namba 60 kilichopo Regent Estate, Kata ya Mikocheni, wilayani Kinondoni kati ya mfanyabiashara, Ghalib Said Mohamed (GSM) na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, unazidi kufukuta baada ya kila mmoja kudai ni mmiliki halali.

Je, kati ya GSM na Makonda nani ni mkweli kuhusu umiliki halali wa eneo hilo?

Fukuto la mgogoro huo limeibuka hadharani kwa mara ya kwanza baada ya Makonda kuonekana wiki iliyopita kupitia video fupi zilizowekwa katika mitandao ya kijamii akiwa eneo hilo huku akidai kwamba kila kilichopo hapo ni mali yake na viongozi wanaosimamia sheria wanajua nani ni mmiliki wake halali.

Pamoja na mambo mengine, Makonda, anasikika akilalamika kupitia video hizo akiwalaumu kina GSM kwamba wameamua kutumia watu wengine kumdhalilisha mitandaoni kwamba anataka kudhulumu na akawataka waendelee na yeye hatajali.

“Watakapomwita, atakapokuja ataeleza utapeli anaofanya na ‘finally’ viongozi wanaosimamia sheria wanajua nani mwenye mali na ukishajua nani mwenye mali kinachofuata ni chepesi tu, kukabidhi mali,” amesema na kuongeza:

“Nimewaambia kama kampuni za ulinzi ninazo, nisingeshindwa kunyanyua simu na kuomba askari 30 wakaja hapa na hata wao wasingegusa lakini wameingia ‘smooth’ kama vile eneo ni la kwao na tulikuwa tunaendelea kusubiri taratibu wao wana ‘advance’.”

Katika hatua nyingine, amenukuliwa baada ya kuulizwa na gazeti moja linalochapishwa kila siku akisema: “GSM, usinilazimishe kusema uozo wako, achia mali yangu. Walioko nyuma yako nawajua.”

Pia mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Makonda, ameweka video ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, akisema kuna haja ya Jeshi la Polisi kuchunguzwa.

“Naunga mkono hoja ya Kamati Kuu ya kuchunguza mwenendo wa baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi, wanaolipaka tope Jeshi la Polisi kwa kuwalinda wafanyabiashara matapeli wanaodhulumu mali za watu. Naomba tuanze na Dar es Salaam na mimi Paul Makonda niko tayari kutoa ushirikiano,” amesema.

Wakati Makonda akisema hivyo, Wakili wa GSM, Alex Mgongolwa, ameonyesha hadharani vielelezo vya umiliki wa eneo la kiwanja hicho. 

Mgongolwa amezungumzia mgogoro huo mwishoni mwa wiki iliyopita na akamtaka mtu mmoja ambaye hakutaka kumtaja jina, kuweka wazi vielelezo vya umiliki alivyonavyo vya eneo hilo pamoja na vile kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi vinavyompa uhalali wa kulimiki.

Pia amesema mteja wake, GSM, alinunua ardhi hiyo Novemba 21, 2006 wilayani Kinondoni kwa lengo la ujenzi wa makazi.

“Mteja wangu alinunua eneo la Regent Estate plot no. 60, title no. 186153/60. Pia Septemba, 2017, aliingia mkataba na Kampuni ya ujenzi ya Group Six International (Contract Class One) kwa ajili ya ujenzi wa eneo hilo wenye thamani ya Sh milioni 640,” amesema na kuongeza:

“GSM aliomba kibali cha ujenzi na Manispaa ya Kinondoni walikitoa Oktoba 16, 2017 chenye kumbukumbu namba 00020032 kwa Ghalib Said Mohammed kwa ajili ya ujenzi.” 

Baada ya kibali hicho kutoka, amesema kampuni hiyo ilianza ujenzi kisha Januari 31, 2018 wakapeleka malipo ya awali huku mteja wake akitekeleza sehemu ya mkataba kwa kulipa Sh milioni 51.92 zilizothibitishwa pia na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Leo (Jumamosi ya wiki iliyopita) nathibitisha uhalali wa miliki. Unaweza ukawa na uhusiano na mtu lakini si wa biashara ya kuuziana na kuhamishiana miliki licha ya kuingia makubaliano,” amesema.

Pia amesema kufahamiana na mtu ni jambo jingine na miliki ni jambo jingine na ushahidi wa kisheria unakingwa na vielelezo hivyo.

“Sasa tunatoa changamoto kwa yeyote yule aje apingane na vielelezo vyetu, huu ni ujenzi kwa mujibu wa mkataba na haujasimamiwa na mjomba au shangazi,” amesema na kuongeza:

“Yeyote yule anayesema ardhi ni ya kwake aje na vielelezo kwetu, mtu mwenye dhana tofauti milango ya mahakama iko wazi na kwa sasa hatutakwenda mahakamani.

“Hatua tutakazozichukua kuanzia sasa itategemea na matukio yatakayofuata kwa kuwa yatatupa mwongozo wa nini tukifanye. Ikitokea ya kwenda mahakamani, tutakwenda; ikitokea kuangalia ngazi nyingine, tutalipeleka kwa kuwa maelekezo yetu yako wazi, tunatakiwa kulinda haki ya mteja wetu sambamba na jina lake,” amesema.

Wakili atoa elimu mgogoro  wa GSM, Makonda

Katika hatua nyingine, Wakili Bashir Yakub, ametoa elimu kutokana na mgogoro unaoendelea kati ya GSM na Makonda kwa kusema kuwa mtu yeyote yule akinunua nyumba, kiwanja au shamba anapaswa kuhakikisha anahamisha miliki kutoka kwa muuzaji kwenda jina lake haraka kadiri atakavyoweza.

Amesema watu wengi wanafanya kosa (wanaponunua ardhi, nyumba au shamba kwa sababu hakuna anayemlazimisha) kutohamisha miliki kwa haraka na wakishakabidhiwa hati na mikataba ya mauziano wanakaa nazo hata miaka miwili au mitatu wakisubiri wapate fedha ndipo wafanye hivyo.

Ametahadharisha kuwa kama mnunuzi hajahamisha miliki kuna uwezekano mkubwa kwa muuzaji akamzunguka.

“Mfano mmoja ni kuwa aliyekuuzia anaweza kutoa taarifa ya kupotelewa hati, hivyo kupatiwa taarifa ya kupotea (lost report).

“Kisha akatoa tangazo katika gazeti la kawaida na lile la serikali na akafanya maombi ya kupatiwa hati mpya kupitia fomu namba tatu chini ya Kifungu cha 38 cha Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura ya 334. 

“Kisha akapatiwa hati nyingine mpya. Kwa hiyo kutakuwa na hati mbili katika ardhi moja, ile aliyompa mnunuzi na mpya ya kwake. Huu tayari ni mgogoro mkubwa kwako mnunuzi usiye na hatia,” amesema.

Bashir amesema muuzaji akishakuwa na hati hiyo ni dhahiri anaweza kuyakataa mambo mengine kwa urahisi na pengine watu wa namna hiyo hata zile saini anazoweka katika nyaraka nyingine zinakuwa si zake. 

Amesema kibaya zaidi mnunuzi asipohamisha miliki na wakati ameshanunua, shughuli zote zinazohusu ardhi hiyo, mfano kulipia kodi za ardhi, vibali vya ujenzi, tathmini, tozo na kila kitu kinaendelea kusoma jina la muuzaji na kinafanyika kwa jina lake.

“Maana yake ni kwamba, ushahidi wote wa risiti na nyaraka nyinginezo unaendelea kumtambua muuzaji kuwa mmiliki halali na anaweza kutumia ushahidi huo dhidi ya mnunuzi,” amesema na kuongeza: 

“Ataonyesha risiti zinamsoma yeye muuzaji na atasema alikuwa analipia, atachukua hata kibali cha ujenzi bila wewe kujua na atakionyesha kinamsoma yeye. Kushinda kesi ya namna hiyo anahitaji tu kudra za Mungu kama atabahatika kuzipata.

“Lakini kama mnunuzi amehamisha miliki, mchezo huu ni mgumu na hauwezekani, hata ukiwezekana kwa nguvu ya rushwa ama mamlaka, bado unaponyeka (curable) kwa sababu mfumo huonyesha umiliki ulivyokuwa ukihama hadi mmiliki wa mwisho.”

Amewashauri wanunuzi wa ardhi, mashamba au nyumba kufanya haraka uhamisho wa miliki na wasiogope kulipa asilimia 10 ya gharama ya ‘capital gain’ kwa sababu inapungua baada ya kufanya mazungumzo. 

“Mna uhuru wa kuchagua kati ya shari kamili ya kudhulumiwa ardhi yote au nusu shari ya hiyo asilimia 10 ya capital gain. Wanunuzi nao wanatakiwa kuhakikisha mikataba yao inashuhudiwa na mawakili.

“Kwa sababu anakuwa ni nguzo muhimu katika mgogoro wa ardhi, nyumba au shamba, kwa kuwa wakili kwa cheo chake ni ofisa wa viapo (commissioner for oaths), ni mthibitishaji wa umma (notary public), pia ni ofisa wa mahakama, na akiwa katika mkataba wako ni mtu muhimu na shahidi wako anayeaminiwa mahakamani,” amesema.