‘Sniper’ wa tembo atupwa jela

*Hukodiwa kwa Sh 300,000 kuua tembo mmoja

*Ni mtaalamu wa shabaha, mkazi wa Kibiti, Pwani

MARA

Na Mwandishi Wetu

Huku akiwa bado anatumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kosa alilokutwa nalo mwaka 2017, Karimu Musa (40), maarufu kwa jina la ‘Mbweha’ amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.

Mbweha ni mdunguaji na mtaalamu wa kulenga shabaha (sniper) aliyekutwa na hatia baada ya kukamatwa na wenzake watatu akiwa amekodiwa kwa kazi hiyo akitokea Kibiti mkoani Pwani.

Machi 4, mwaka huu, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, Adelina Mzalifu, amewahukumu Mbweha pamoja na wenzake watatu wakazi wa vijiji vya Robanda, Katembere na Bwitengi, Serengeti, mkoani Mara; Khamisi Gamaho (37), Hamisi Mabula (52) na Ginena Bwanana (34), kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja, baada ya kuwakuta na hatia ya kushiriki vitendo vya ujangili.

Wote kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 3/2018.

‘Mfungwa’ alivyoshiriki ujangili

JAMHURI limethibitishiwa na polisi, maofisa wa TANAPA na Ofisi ya Mashitaka kuwa mwaka 2017, Mbweha, mdunguaji na mtaalamu wa shabaha, alikamatwa mkoani Mwanza akisafirisha bunduki kutoka Dar es Salaam kwenda Mara kwa ajili ya ujangili. 

“Kesi yake ilifanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma chini ya Ofisi ya Mashitaka na akafungwa miaka mitatu jela.

“Lakini inavyoonekana mtandao wake ulicheza ‘mchezo mchafu’ kwani baadaye kifungo chake kikabadilishwa na kuwa cha nje. Akahamishiwa Dar es Salaam na kutakiwa kutumikia jamii huko,” amesema.

Hata hivyo, badala ya kwenda Dar es Salaam ‘kutumikia jamii’, Mbweha, kwa kutumia mtandao wa ujangili, akikubalika na kuaminika kuwa mdunguaji mahiri mwenye shabaha ya ajabu kutokana na uzoefu wa uwindaji na ujangili; akabaki ‘kazini’.

Taarifa zinasema kwamba Mbweha alikuwa akikodiwa na kulipwa Sh 300,000 kwa kila mnyama anayemuua.

“Baada ya kukamatwa ndipo ikabainika kuwa huyo alikuwa mfungwa ambaye hata kubadilishiwa kifungo kuwa cha nje kwa kosa la kusafirisha bunduki bila kibali kwa ajili ya ujangili kuliibua maswali mengi yasiyokuwa na majibu,” amesema ofisa wa Tanapa jina limehifadhiwa.

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Mara, Yese Temba, ameliambia JAMHURI akisema: 

“Kwa mujibu wa sheria, kifungo cha miaka mitatu kinaruhusiwa kubadilishwa na kuwa kifungo cha nje. Kuhusu kesi ya awali na ilikuwaje, nipe muda nifuatilie kwenye majalada.”

Hata hivyo, Temba hakuonyesha tena ushirikiano na JAMHURI kwani kila alipokuwa anakumbushwa kwa kupigiwa simu au kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, amekuwa akidai kuwa hajapata nafasi ya kufuatilia.

Bunduki iliyoua tembo ilivyosafirishwa

Uchunguzi wa JAMHURI umeibaini kuwa Desemba 30, 2017, mmoja wa majangili hao, Bwanana, alisafarisha bunduki aina ya ‘Rifle 458’ kwa basi la abiria liitwalo Natta Raha ikiwa ndani ya mzigo wa mahindi ya kuchoma hadi Kijiji cha Robanda ilikopokewa na mke wa Gamaho.

Silaha hiyo inadaiwa kuingizwa na mratibu wa mtandao (jina tunalihifadhi kwa sasa kwa kuwa hatujazungumza naye) ambaye ni mwenyeji wa Robanda na Bwitengi.

Kwa upande mwingine, mratibu wa mtandao alipeleka risasi zilizotumika katika ujangili katika Kijiji cha Robanda ambako Mabula alizipokea.

Inadaiwa kuwa Mei 2017, Mabula na Bwanana walishirikiana kuua tembo katika Pori la Akiba la Ikorongo.

Timu ya ujangili ikakamilika Desemba 30, 2017 baada ya kuwasili kwa ‘mtaalamu’ Mbweha kijijini Robanda na kupokewa na Gamaho; tayari kuingia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Siku moja baadaye, yaani Desemba 31, 2017 wakati wananchi na raia wema wakishangilia mkesha wa mwaka mpya, timu hiyo ilikuwa ndani ya hifadhi na kuua tembo wawili wakubwa kwa risasi mbili tu.

Januari 2, 2018 wakati shamrashamra za mwaka mpya zikianza kupoa, wao wakaingia kijijini wakiwa na meno manne ya tembo; wakayafukia kwenye mchanga wa kujengea nyumbani kwa Gamaho.

Walikutwa wamelala ‘mzungu wa nne’

Mmoja wa maofisa wa polisi aliyeshiriki operesheni ya kuwakamata ameliambia JAMHURI kuwa usiku wa siku hiyo ya Januari 2, 2018, walipata taarifa za kuuawa kwa tembo wawili na kwamba meno manne yamehifadhiwa nyumbani kwa Gamaho, Robanda.

“Kesho yake saa nne asubuhi tulifika kijijini hapo na kuwataarifu wenzetu wa TANAPA. Tukaunda kikosi kimoja kwenda kuwakamata. Tuliwakuta wamelala sebuleni ‘mzungu wa nne’; ishara kuwa usiku walikuwa na kazi nzito maalumu,” amesema.

Baada ya mahojiano ikabainika kuwa watu hao wanne wamekutana kwa kazi maalumu, wakitoka maeneo tofauti; Mabula anatoka Ketembere, Kata ya Rigicha; Bwanana (Bwitengi – Kata ya Manchira) huku Mbweha akitokea Mwaseni, Kibiti mkoani Pwani.

Mbweha azimia 

Ofisa huyo anahadithia: “Tukawatoa nje kwa mahojiano. Mbele ya nyumba kulikuwa na mchanga wa kujengea ulioonekana kama umevurugwa.

“Wakati mahojiano yakiendelea, ofisa wetu mmoja, bila kutarajia, akawa anachomachoma kwa mti kwenye ule mchanga; akakutana na meno manne ya tembo! Kitendo kile kilimshtua na kumfadhaisha Mbweha kiasi cha kuzimia.”

Ugomvi wa mke wasaidia Serikali

Baada ya kugundua kufichwa kwa meno ya tembo mchangani, kikosi cha maofisa wa Polisi na TANAPA kikahamisha mahojiano na sasa kikataka kujua ilipo silaha iliyotumika kuua tembo hao.

Askari polisi aliyeshiriki mahojiano hayo analiambia JAMHURI kuwa pamoja na meno ya tembo kukutwa kwenye himaya yao, watuhumiwa hawakuwa tayari kueleza ilipo bunduki.

“Kwa bahati nzuri Gamaho hakuwa kwenye uhusiano mwema na mkewe, hivyo mama huyo (jina tunalihifadhi) akatoboa siri na kuonyesha walikokuwa wamehifadhi hiyo silaha,” amesema.

Baada ya kubanwa sana wote wanne wakakiri kuhusika na mauaji ya tembo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kikosi kizima na watuhumiwa wakasafiri hadi ndani ya hifadhi kutaka kuona mizoga ya tembo.

Hata hivyo, kikosi hicho kilipelekwa na kuonyeshwa mzoga wa zamani, hivyo kulazimika kuwabana zaidi watuhumiwa na ndipo wakaonyesha mizoga miwili ya tembo waliouawa siku chache tu nyuma.

Mwingine alikuwa anasakwa kwa kumiliki bunduki

JAMHURI liliambiwa kuwa Hamisi Mabula mkazi wa Ketembere alikuwa anatafutwa kwa tukio jingine la kuwajeruhi wenzake kwa risasi porini wakati wakiwinda kisha kuwapora nyama walizokuwa wamewinda ndani ya Pori la Akiba la Grumeti.

Mabula baada ya kukamatwa, waliodai kujeruhiwa walijitokeza na alipobanwa, akawapeleka maofisa wa serikali na askari polisi ndani ya Pori la Akiba la Grumeti eneo la mto na kufukua bunduki aina ya AK 47 na risasi 130; vyote vikiwa ndani ya mfuko wa nailoni.

Hapo ndipo lilipokuwa ghala lake la silaha na kila baada ya kumaliza ujangili, huhifadhi hapo silaha na risasi.

Huku tayari akiwa anatumikia kifungo cha miaka 20 jela, Wakili wa Serikali, Donasian Chuwa, anasema Mabula anakabiliwa na kesi nyingine namba 37/2022 katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti ya kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria. Kesi hiyo itatajwa Machi 17, mwaka huu.

Uchunguzi wa JAMHURI uliothibitishwa na vyanzo mbalimbali vya habari ulibaini washitakiwa wote wamekuwa kwenye mtandao wa ujangili kwa muda mrefu.

Mwaka 2017, Gamaho alimaliza kifungo kwa kosa la kukamatwa na bunduki na mafuta ya nyamela huku Bwanana pia akiwa amewahi kukamatwa kwa makosa ya ujangili.

Kijiji chalaani mauaji ya tembo

Katika mkutano wa Kijiji cha Robanda uliofanyika Januari 13, 2018, Mwenyekiti wa Kijiji, Mrobanda Japani, aliwataka wananchi kutompokea mratibu wa mtandao (anamtaja jina) wa ujangili, vinginevyo watahamishwa kwa kuwa amewakosea kuua tembo anayeabudiwa kama mungu wao.