Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkoa wa Pwani umeendelea kutekeleza kwa mafanikio Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku ongezeko la makusanyo ya mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na halmashauri likiimarisha uwezo wa serikali wa kugharamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii.

Katika mwaka wa fedha 2025/2026 hadi Machi 31, 2026, TRA Mkoa wa Pwani ilikadiria kukusanya Sh bilioni 189.645 kutoka kodi za ndani na forodha, lakini ilifanikiwa kukusanya Sh bilioni 216.029, sawa na asilimia 113.91 ya lengo.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, kwa Halmashauri Kuu ya Mkoa, Kamisaa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema utekelezaji wa ilani unategemea upatikanaji wa fedha.

“Utekelezaji wa ilani ni fedha, huwezi kutekeleza ilani bila kuwa na fedha, Hivyo mkoa unaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha usimamizi wa vyanzo vilivyopo “;alisema Kunenge.

Kunenge alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri za Mkoa wa Pwani ziliidhinishiwa kukusanya Sh bilioni 87.96, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 14.503 kutoka Sh bilioni 73.454 zilizokadiriwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 19.74.

“Hadi kufikia Machi 2026, jumla ya Sh bilioni 92.419 zilikuwa zimekusanywa, sawa na asilimia 105.07 ya lengo, kufikia Mei 31 mwaka huu, tumevuka lengo jipya la makusanyo kwa kukusanya Sh bilioni 109.7, sawa na asilimia 115.1, Hii ndiyo Pwani ambayo sasa ni mkoa wa pili kitaifa kwa ukusanyaji wa mapato,” alifafanua Kunenge.

Pia mkoa huo unaendelea na utekelezaji wa mipango katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, kilimo, uvuvi, utalii, uwekezaji, maji, nishati, TEHAMA, michezo, usafirishaji na miundombinu ya barabara.

Hata hivyo, Kunenge alisema baadhi ya barabara zimeharibika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni, lakini serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuchukua hatua za kudhibiti au kuondoa changamoto hiyo.

Akifunga mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, aliwataka viongozi kulinda ardhi na kujiepusha na vitendo vya kushiriki au kuchochea uuzaji holela wa ardhi za vijiji na maeneo mengine .

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibiti, Juma Ndaruke, alipongeza uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani pamoja na usimamizi wa utekelezaji wake unaofanywa na uongozi wa mkoa.