Tanzania, Rwanda na Burundi zaanza kupata umeme kutoka Rusumo

Mradi kuzinduliwa mwezi Machi 2024, Dkt. Biteko ataka ukamilike mapema

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa maporomoko ya umeme wa Rusumo wa megawati 80 unaotekelezwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi umefikia asilimia 99.9 na nchi hizo tayari zimeanza kupata umeme kutoka kwenye mradi huo.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 18 Desemba, 2023 jijini Mwanza wakati akiongoza kikao cha ngazi ya Mawaziri wa Nishati ambaye yeye ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa wanaosimamia mradi huo kutoka nchi hizo Tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi.

” Tumeridhishwa na maendeleo mazuri ya mradi mpaka sasa, tunawapongeza Bodi na Watendaji kutoka kampuni ya umeme ya Rusumo na wakandarasi kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huu.” amesema Dkt. Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati wa kikao cha ngazi ya Mawaziri wa Nishati kutoka nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi kuhusu mradi wa umeme wa Rusumo
kilichofanyika jijini Mwanza tarehe 18 Desemba, 2023. ambao wanasimamia mradi huo.

Dkt. Biteko amesema Mawaziri hao wamekubaliana kuwa, mradi huo uzinduliwe mwezi Machi mwaka 2024 hivyo wamemtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo mapema na atoe cheti cha kukamilisha mradi.
Amesema uzinduzi huo utafanyika katika eneo la mradi huku mwenyeji wa shughuli hiyo akiwa ni Tanzania.

Amesema kuwa, mradi huo una umuhimu kwa nchi zote tatu kwani badonnchi hizo zina changamoto ya upatikanaji wa uhakika wa umeme hivyo kukamilika kwa mradi huo kutapunguza changamoto hizo na kuongeza uimara kwenye gridi.

Dkt. Biteko amewashukuru Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame kwa msukumo wanaotoa katika utekelezaji wa mradi huo ambao umepelekea kufikia asilimia 99.9.

Vilevile, Dkt. Biteko ameshukuru wadau mbalimbali waliopelekea mradi huo kutekelezwa ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Afrika ( AfDB) na amewakaribisha kuwekeza kwenye miradi mingine ya uzalishaji umeme inayotarajiwa kutekelezwa nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mafuta, Nishati na Migodi wa Burundi, Mhandisi Seleman Khamissi ambaye alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo amesema kuwa, nchi zote Tatu zimekubaliana kuwa mradi huo uzinduliwe mwezi Machi na kwamba nchi hiyo itafaidika na megawati 27 zitakazotoka kwenye mradi huo ambao utasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji umeme kwenye nchi hiyo.

Kutoka Rwanda kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Miundombinu, Dkt. Jimmy Gasore ( ambaye alishiriki kwa njia ya mtandao) na kutoka Tanzania, viongozi waliohudhuria ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Mwenyekiti wa wa Bodi ya Kampuni ya Umeme ya Rusumo.

Mradi wa umeme wa Rusumo utazalisha megawati 80 ambapo kila nchi itapata megawati 27 za umeme.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mafuta, Nishati na Migodi wa Burundi, Mhandisi Seleman Khamissi (wa Pili kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kutoka Tanzania, Mhandisi Felchesmi Mramba (wa Pili kulia) wakati wa kikao cha ngazi ya Mawaziri wa Nishati kutoka nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi kuhusu mradi wa umeme wa Rusumo kilichofanyika jijini Mwanza tarehe 18 Desemba, 2023. ambao wanasimamia mradi huo.

By Jamhuri