Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Maandalizi ya utunzaji wa historia ya Hospitali ya Taifa Muhimbili tangu enzi za Sewahaji hadi sasa yameanza ambapo leo Uongozi wa Makumbusho ya Taifa umekutana na Uongozi wa hospitali kujadili namna nzuri ya kushirikiana kutekeleza jambo hilo kabla ya ujenzi mpya kufanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi amemueleza Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga kuwa, upembuzi yakinifu kuhusu mradi huo unaratajia kuanza mapema mwakani ambapo katika ujenzi huo, utunzaji historia ni kipaumbele namba moja, baadhi ya majengo yatabaki na mojawapo litakuwa makumbusho ili kulinda historia yake kwa vizazi vijavyo kuhusu hatua moja hadi nyingine ambazo Taifa limepitia katika mapinduzi ya utoaji huduma katika sekta ya afya nchini.

“Hospitali ina majengo mengi ya zamani, yanayohitaji ukarabati mkubwa na kutokukidhi mahitaji ya sasa ya utoaji huduma hivyo tunahitaji kuijenga upya, katika hilo tutazingatia mambo mengi ikiwemo kuweka huduma karibu ili kupunguza usumbufu kwa wagonjwa kutembea mita 500 kufuata kipimo flani au huduma nyingine sehemu flani” amesisitiza Prof. Janabi.

Amesema, ujenzi huu utazingatia matumizi sahihi ya ardhi ambapo eneo kubwa litakuwa wazi baada ya ujenzi huo kwani majengo yatakuwa machache ukilinganisha na hali ilivyo sasa, kutakuwa na ramani moja (comprehensive plan), kukidhi vigezo vingi vya kimataita vya utoaji huduma, kuboresha na kuongeza huduma za kibobezi, kuwa kituo cha mafunzo ya huduma za ubobezi na kuifanya Hospitali kuwa kituo cha Utalii Tiba (Medical Tourism Hub).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Lwoga ameipongeza Menejimenti ya hospitali kwa kutambua umuhimu wa kuhifadhi historia ya taifa kwa ajili ya vizazi vijavyo na kuahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kutimiza azma hiyo.

“Sisi kama makumbusho ya taifa pamoja na mambo mengine tuna jukumu la kuhakikisha kuwa tunahifadhi historia ya nchi yetu, kutoa ushauri na elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi historia ya kale kwa ajili ya vizazi vijavyo” amesema Dkt. Lwoga.

Dkt. Lwoga amesisitiza kuwa kuhifadhi historia ya kale hakuzuhii maendeleo yasifanyike bali ni kuhakikisha maendeleo hayo yanaenda sambamba na utunzaji wa historia ya nchi yetu.

“Hospitali ya Taifa Muhimbili ikihifadhi historia yake, sekta ya afya itakua na kitu cha kujivunia kuonesha hali ilivyokuwa tangu kabla na baada ya ukoloni na kukifanya kizazi kijacho kuona hatua mbalimbali za maendeleo zilizofikiwa kisekta chini ya awamu tofauti za uongozi” amesema Dkt. Lwoga.

By Jamhuri