Ndugu Rais, sikutaka kuandika lolote kwa kinachoitwa kumbukizi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kila inapofika Oktoba 14, kila mwaka kwangu huwa ni siku ya kuomboleza na kulia sana.

Hii ndiyo siku ya majonzi na simanzi kubwa Taifa limepata kushuhudia. Siku ya kihoro! Siku mshumaa uliokuwa unamulika kuiondoa giza katika nchi hii ulipozimika.

Tangu siku hiyo giza totoro limeifunika nchi yetu nayo sasa nchi inaongozwa kwa kupapasa! Watanzania walilia na Taifa zima liliomboleza lakini Mwalimu, Baba wa Taifa alienda! Wanasema kazi ya Mungu haina makosa, mimi siamini!

Hata alipokuwa katika kitanda chake cha mauti akisubiri kuitoa roho yake arejee kwa Muumba wake na katika mateso yakufifisha kama yale, Julius Kambarage Nyerere hakutusahau wanawe, wana wa Taifa hili Tanzania. Maneno yake ya mwisho alimwambia kijana wake, kaka yetu mkubwa Rais Benjamin William Mkapa akasema, “Najua kwa ugonjwa huu siponi. Najua Watanzania watalia sana! Lakini kawaambie, nitakwenda kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu!’’ Julius Kambarage Nyerere akarudi kwa Muumba wake. Yaliyoje mapenzi makubwa hayo?

Mhariri wangu kaniambia usipoandika lolote wanawema wanaweza wasituelewe. Nikawaza niandike nini? Vidole vyangu vimelegea nitaandikia nini? Nitaiweka wapi karatasi yangu ya kuandikia ili isilowe kwa machozi yanayonitiririka bila kizuizi? Mwalimu Nyerere ametangulia kaka zangu wanamfanyia dhihaka! Lakini hata wewe Joseph Butiku? Basi, Julius Kambarage Nyerere kapumzike kwa amani! Katika kukua kwangu kote na sasa nimekuwa mzee sijawahi kushuhudia watu wakipumbazwa mpaka wakaifanya siku waliompoteza mkombozi wao kuifanya ‘Holidei’. Inauma sana!

Wanamtukuza Mwalimu Nyerere siku aliyokufa! Siku Baba wa Taifa aliyozaliwa viongozi wote wanaijua! Hii haifanyiki kwa bahati mbaya. Siku zitapita, lakini siku zitakuja watakapokuja viongozi wasio na unafiki, nao watamuenzi Baba wa Taifa siku stahili!

Wanawema niandike nini Mwalimu Nyerere ameishaenda? Wamekuja wanaomfukuza jogoo. Wanavyoona wao ndivyo wanavyotaka wananchi. Wanavyofikiri wao ndiyo maoni ya wananchi. Lakini hawataki siku moja wananchi nao waje wale vya kunona kama wanavyokula wao na watoto wao! Inauma sana!

Tusome ya zamani katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Mtukufu sana Rais, mwananchi atamchokaje mtawala wake? Mwananchi ni mtu wa kuambiwa fanya hivi na lazima afanye, atake asitake. Akiambiwa kula majani ni lazima ale majani. Wananchi wa nchi hii na hasa wa vijijini wana nafasi gani katika kuiendesha nchi hii? Wao wasubiri kuongozwa tu. Mawazo yetu sisi viongozi ndiyo maoni yao wao wananchi.’’

Rais Nyerere aliamini katika maendeleo ya watu siyo maendeleo ya vitu. Hakuwafanyia miradi mikubwa ambayo haikugusa maisha yao, bali aliwawekea dawa za kuwatibu katika Hospitali zao. Hakuwambia wananchi kuwa aliwasomesha watoto wao bure. Hata hivyo, hakuna watoto waliorundikwa chini eti kwa sababu hakukuwa na malipo ya ziada. Aliweka watoto 45 kila darasa. Kujimwambafai kuwa tunawafanyia wananchi miradi mikubwa kutakuwa hakuna maana kama tutafanana na mafisadi waliochukua fedha za wananchi wakazitumia kwa manufaa yao wakiwaacha wamepigika vibaya na sisi tunazichukua fedha hizo hizo tunawanunulia viberiti vya chuma ambavyo hawavihitaji.

Hospitalini wakienda wanaandikiwa dawa wakanunue. Wanadaiwa malipo makubwa kwa huduma wanazopatiwa hata kushindwa kukomboa maiti wa wafu wao.

Niliandika haraka ili niwahi kuzika. Nyumba ya nne kutoka kwangu alikuwako ajuza aliyekuwa anaishi kwa mjukuu wake. Alibahatika kupata mtoto mmoja tu wa kike ambaye hayupo. Binti naye alikuwa na mtoto mmoja tu wa kike ndiye alikuwa anaishi na bibi yake. Nikiongea naye bibi yule nilimkumbuka marehemu mama yangu. Nimeambiwa amefariki dunia.

Naambiwa alikosa huduma. Alikuwa anakohoa sana. Kila alipoenda hospitali ya serikali hapa kwetu Mbagala Zakhem aliandikiwa dawa ambazo kumbe kwa sababu ya umasikini wake alikuwa hawezi kuzinunua. Mjukuu anaishi kwa kuuza kachori za shilingi hamsini hamsini. Bibi alikohoa mpaka mbavu zikagandamana, sasa amefariki! Inauma sana!

Msibani yalisemwa mengi. Wakakumbusha mamilioni wanayoona yanatawanywa katika kila barabara tunazopita. Mamilioni yanatawanywa mpaka nchi za nje ambako huko wenzetu hospitali zao zimejaa dawa. Inauma sana! Muasisi wa vyama vingi ameenda waliomfuatia wanamfukuza jogoo. Wanafana na wale wanawali 15 wapumbavu hawakuchukua mafuta ya akiba, lakini watano wenye busara waliochukua mafuta ya akiba. Viongozi wanaotaka madaraka wanafanana na wanayemtaka jogoo kwa kitoweo.

Wasio na busara huamua kumfukuza jogoo wakijua watamkamata. Katika mbio zao jogoo akipanda tuta nao wanapanda tuta. Jogoo akiingia katika dimbwi la maji machafu na wenyewe wanaingia katika dimbwi la maji machafu. Akiteremsha na wenyewe wanateremsha. Akipandisha na wenyewe wanapandisha. Jogoo akijisweka katikati ya miiba na wenyewe wanataka kujisweka humo. Mwishowe jogoo yuko hoi anatoka damu na wenyewe wako hoi wanatoka damu. Jogoo hajakamatwa! Hawa ni baadhi ya viongozi mufilisi wanaodhani dawa ya vyama vya upinzani ni kuvinyamazisha au kuvifuta.

Viongozi wenye busara wakimtaka jogoo, huingia ndani na kutoka na punje za mahindi wakaita, kuku, kuku, kuku huku akizimwaga zile punje za mahindi mpaka kwenye miguu yao. Kuku humkimbilia na kuanza kugombania punje za mahindi. Taratibu atainua mguu wake na kuukanyaga mguu kwa nguvu jogoo anayemtaka. Kuku wanapotawanyika atainama chini na kumchukua jogoo wake! Hawa ndiyo viongozi wenye busara kubwa kama Rais Uhuru Kenyatta aliyejiimarisha kiuongozi kwa kuimarisha upinzani.

Wakati kiongozi anafikiria kuunyamazisha upinzani kwa kuufuta, kiongozi mwenye busara huuona upinzani kama kioo kinachomuonyesha matongotongo aliyonayo usoni. Hivyo atasafisha uso wake na atakisafisha na kioo.

Ni nani anasikia siku hizi wapinzani nchini Kenya wananyanyaswa na serikali au kukamatwa na kufunguliwa kesi za kipuuzi? Wanaruhusiwa kuandamana kupinga wasichokitaka, lakini nani anaandamana? Pakusemea wanapo! Tunayoyashuhudia leo hapa kwetu yanathibitisha kuwa baadhi ya viongozi wetu wana fikra za kumfukuza jogoo. Inauma sana. Na kwa ufunuo wa Balozi Wilbrod Slaa, jogoo wetu ametuingiza katikati ya michongoma yenye miiba mikali. Hatoki mtu bila kutoka damu! Mwenye masikio ya kusikia na asikie.

By Jamhuri