Sehemu ya kwanza, nilieleza kuwa wanahistoria wanasema hadi karne ya 17 (miaka ya 1600 AD), duniani hapakuwapo kitu kinachoitwa au kinachojulikana kama CHAMA CHA SIASA tangu enzi za Wagiriki. Endelea….

 

Enzi za utawala wa Warumi (The Roman Empire) kulikuwa na mfumo wao wa utawala ambao haukuwa tofauti na ule wa Wagiriki. Warumi nao walikuwa na mfumo wa wawakilishi. Nao makundi yao yalikuwa mawili.

Kundi la watu mashuhuri ukoo wa watawala (emparors) na wanajeshi na kundi la matajiri – mabepari kama vile katika hadithi ya “The Merchant Of Venice” akina “Shaylock”. Hivyo, utawala wa Warumi ulikuwa wa matabaka – wenyenacho waliunda seneti ya kujadiliana namna ya kulinda maslahi yao. Akina kabwela waliunda kikundi chao ili kujadili namna ya kudai haki zao kutoka kwa watawala na matajiri. Tunaona pia makundi mawili yenye maslahi tofauti kabisa. Bado makundi yale hayakuitwa vyama vya siasa.

Nchini Uingereza nako tunaambiwa hivyo hivyo kwamba mnamo karne ya 17 hivi ndipo kulizuka chokochoko zilizoanzisha vyama vya siasa. Lakini kule Uiingereza hivyo vyama vya siasa havikutokana na makundi ya walionacho (mabwanyenye) na kundi la wasionacho (makabwela). Kule tunaambiwa makundi yalitokana na imani ya DINI.

Ilikuwa enzi za utawala wa Mfalme Charles II (1660-1685) kulitokea sokomoko lililoanzia kwenye UZUSHI uliosambazwa na Mwingereza aliyeitwa Titus Oates ambaye aliwahi kuwa Kasisi wa Kanisa la Anglikana, lakini aliachishwa ule ukasisi (a renegade Anglican priest).

 

Huyu Titus alizusha na kueneza habari kuwa kulikuwa na mpango katika Kanisa Katoliki ulioandaliwa rasmi wa kumuua Mfalme Charles II na kisha kumteua mwana mfalme James aliyekuwa Duke of York ambaye alikuwa ni mdogo wake huyo Mfalme Charles II.

 

Uzushi ule ulijulikana kule Uingereza kama “THE POPISH PLOT” katika historia ya siasa za Uingereza na ulisambazwa kati ya Agosti 12 na Septemba 28, 1678. (soma hayo toka Encyclopaedia Britannica Vol. 16 uk. 815).

Ikumbukwe kuwa Uingereza ni nchi ya madhehebu ya Anglikana kuanzia enzi ya utawala wa Mfalme Henry VIII (1491 – 1547). Huyu Mfalme Henry VIII licha ya kuwa Mkatoliki, ndiye aliyetofautiana na Papa wa Roma juu ya mambo ya NDOA. Basi, mfalme alivunja uhusiano na Roma Desemba 17, 1538 na ikajitenga kuwa nchi yenye madhehebu yake na akayaita ANGLIKANA -dini rasmi ya Uingereza na yeye ndiye akawa Kiongozi Mkuu wa Madhehebu hayo. Hii ilitokea enzi za Upapa wa Paulo III (1534-1549). (Soma zaidi juu ya Mfalme Henry VIII katika Gazeti la Kiongozi toleo No. 24 la tarehe 15 – 21 June, 2018 na matoleo kadhaa yaliyofuata).

Basi, kuanzia Desemba 17, 1538 uhusiano na Roma ulivunjika rasmi. Wafalme wa Uingereza wakawa “automatically” ni Waangalikana na hivyo kuongoza madhehebu hhaya ya Anglikana. Basi, Mfalme Charles II hakuepuka kuwa Mwanglikana.

Kwa kuwa mdogo wake James Duke of York alikuwa bado Mkatoliki, uzushi ule wa Titus ulilenga kuisambaratisha familia ya kifalme, kati ya Waanglikana na Wakatoliki.

Katika Bunge la Uingereza lililokuwa na wajumbe kutoka dini zote mbili, Waanglikana na Wakatoliki kukazuka mjadala wa nguvu kutokana na uzushi ule. Kwa vile wajumbe wengi walikuwa Waanglikana, Bunge likaamua wabunge wale Wakatoliki waondolewe bungeni. Na Wakatoliki wote wenye kazi na nyadhifa serikalini watimuliwe kazi, (huku Tanzania tunasema watumbuliwe).

Na uamuzi wa mwisho wa Bunge lile ulimtaka Mfalme Charles II amfute mdogo wake James Duke of York toka katika ile orodha ya warithi wa Kiti cha Ufalme (from the hereditary line of Royal Family).

Hapo ndipo Mfalme Charles II akaonesha mamlaka yake ya kifalme. Aliwaeleza wabunge kuwa hakubaliani na uamuzi wao kwani uliingilia mamlaka ya ufalme wake.

Mfalme aliunda kamati maalum kufanya uchunguzi wa kina kujua hasa hii “The Popish Plot” ilianzaje, madhara yake na nini kifanyike. (The Popish Plot was planned by the Catholic Church, under the guidance from The Pope in Rome) kwa kusema Kanisa Katoliki lilipanga kumuua Mfalme Charles II ili mdogo wake yule James Duke of York atawazwe kuwa Mfalme wa Uingereza kungekuwa na athari gani.

Jamani, duniani kote binadamu (isipokuwa Kaini kule bustani ya Eden) wanaona damu ni nzito kuliko maji. Hivyo wana ndugu wa ukoo mmoja wana ule mvuto na mshikamano wa damu kuwa ni wamoja kabisa.

Basi kwa ule uzito wa damu moja Mfalme Charles II alikataa kata kata kumwondoa mdogo wake James katika ile orodha ya warithi wa kiti cha ufalme.

Baada ya uchunguzi wa kina ikabainika kuwa uzushi ule wa Titus haukuwa na ukweli wowote. Matokeo yake sasa yalileta mtafaruku katika Bunge la Uingereza.

Msimamo ule wa Mfalme Charles II wa kukataa uamuzi wa Bunge, ulileta mgawanyiko mkubwa usiowahi kutokea katika Bunge lile. Kundi moja la wabunge walimuunga mkono mfalme na kusisitiza kuwa mamlaka ya mfalme yasiingiliwe. Kundi hili lilidai kuwa ile haki ya James Duke of York kurithi kiti cha ufalme (hereditary right of James in spite of his Roman Catholic faith) ni haki yake ya asili na ya kuzaliwa. Kundi hili la wabunge likaitwa “The Torries” maana yake Wakatoliki.

 

Kundi lile la wabunge lililokuwa na msimamo mkali kutokana na uvumi wa Titus lilipinga matakwa yale ya Watori, hili lilidai na kung’ang’ania James Duke of York aondolewe kwenye orodha ya warithi wa taji la kiti cha Ufalme. Hili lilikuwa la Waanglikana, na liliitwa “THE WHIGS” maana yake wapinga uamuzi wa mfalme (wapinzani wapinga Ukatoliki) (Tazama hayo yote katika Encyclopedia Britannica Vol. 23 uk.568).

 

Sasa makundi yale mawili katika Bunge la Uingereza ndiyo yalikuwa asili ya vile vyama vya siasa kule Uingereza viliitwa “Political Parties”. Historia inatuonesha kuwa hii istilahi ya Vyama vya Siasa (this terminology of Political Parties) ndio kwanza inasikika mwaka ule 1678 enzi za utawala wa mfalme Charles II.

 

Ilipofika mwaka 1688/89 kulitokea mageuzi au mapinduzi ya kisiasa (revolution) huko Uingereza. Baada ya mapinduzi yale kimtazamo kule Uingereza, makundi yote mawili “The Torries” na “The Whigs” yenye kuanza kwa mitazamo tofauti ya kidini, tunaambiwa mitazamo yao ikaja kubadilika na kurekebishika (wenyewe wanasema – modified division of principles between the two parties) sasa mitazamo yao kwa umoja wao ililegea na kubadilika – wale “The Torries” wakaja hata kukumbatia itikadi ile ya “The Whigs”.

Kuanzia mwaka 1885 wale waliokuwa wakiitwa “The Torries” ndio sasa wamegeuka kuwa ndio hawa mabwanyenye – “Conservatives”. Historia hii ndugu zangu inatuonesha namna au asili ya vyama vya siasa kule Uingereza tunakowasujudu kama walimu au wasimamizi wa demokrasia duniani.

Basi, katika miaka nenda miaka rudi ya dunia hali Uingereza imefikia hatua ya kuzalisha vyama viwili vikubwa kule hata sisi wa nchi zinazoendelea tunavijua. Kuna chama cha “CONSERVATIVES” na kuna chama cha wafanyakazi kinachoitwa “LABOUR” – hiki kilianzishwa na wafanyakazi mwaka 1900 na kipo pia chama cha waungwana kinachoitwa “THE LIBERALS”. Hiki chama kwa asili yake kilitokana na “The Whigs”. Ni pale ule msimamo mkali “The Whigs” ulipoanza kuyeyuka wenyewe Waingereza wanasema “the evolution from Whiggery to liberalism started roughly around 1815 – 1832” yaani mwanzoni mwa karne ya 19 chama hiki cha “The Liberals” kilianzishwa rasmi (Encyclopaedia Britannica Vol. 13 uk. 1022). Msimamo wa chama hiki cha The Liberals ni rahimu sana.

 

 

 

Itaendelea….

Please follow and like us:
Pin Share