Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Mkoani Pwani Mwalimu Kassim Ndumbo ametoa wito kwa taasisi na mashirika binafsi kushirikiana na serikali katika masuala mbalimbali ya kijamii yakiwemo afya na elimu.

Ndumbo ameyasema hayo wakati alipokuwa akipokea msaada wa chakula na karatasi kwa ajili ya kambi za shule za sekondari kutoka kwa Taasisi ya “Kalamu Education Foundation ” (KEF).

” Ni vizuri kupata wadau wengi zaidi kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha elimu kwa kusaidia wanafunzi wetu wasome vizuri na kufaulu masomo yao” alisema Ndumbo.

Taasisi ya KEF imetoa msaada wa unga viroba 40, mchele viroba 20, maharage viroba 12, mafuta ya kula madumu 5 na karatasi za rim 200. Msaada huu utanufaisha kambi tatu za Shule za Sekondari kwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya kidato cha nne mwaka huu.

Kambi zenye jumla ya wanafunzi 771 wa kidato cha nne wilayani Mafia ni pamoja na Shule za Sekondari Micheni, Kitomondo pamoja na Bweni.