Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Imeelezwa kuwa kitendo cha Serikali ya Awamu ya Sita kukaa meza moja na kujadili mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari nchini,kumeonyesha dhamira njema katika kufanikisha maendeleo ya sekta ya habari nchini.

Hayo yamesemwa na Rais Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari, Deogratius Nsokolo, wakati akitoa maoni yake kuhusu mwenendo wa mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari nchini.

Nsokolo amesema kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amekuwa ni rafiki wa waandishi wa habari.

“Maendeleo yanayopatikana kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari yanatokana na Serikali kuridhia mchakato huo, kwani Rais Samia tangu alipoungia madarakani, alikuwa karibu na sekta ya habari na kutoa matumaini ya kufanyiwa marejeo kwa sheria hi ya mwaka 2016.

“Na tayari matokeo yake ni wadau wa habari Serikali kukaa kwa pamoja na kuainisha vipengele gani tungependa viondolewe,” amesema.

Ameongeza kuwa dhamira hiyo njema inaonyeshwa wazi hasa baada ya wasaidizi wa Rais Samia kuonyesha kwa vitendo hatua kwa hatua katika kukutana na wadau wa habari kwenye vikao vya pamoja na kujadili mchakato huo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema upande wa Serikali na wadau umeishamaliza kazi ya kuainisha vipengele hivyo, kilichotarajiwa ni mwezi wa tisa mwaka huu mapendekezo hayo kupelekwa bungeni lakini kwa bahati mbaya haikuwezekana.

“Serikali kwa uwazi kabisa ilieleza sehemu mkwamo kwamba, mapendekezo hayo hayakufikishwa bungeni kwa kuwa kuna hatua zilikuwa hazijakamilika. Hii ni dhamira ya wazi kabisa ya serikali hii,” alisema.

Alisema, kazi iliyobaki sasa ni upande wa Serikali kukamilisha mchakato na kisha mapendekezo hayo kupelekwa bungeni kwa mujibu wa sheria za nchini.

“Wito wangu, mchakato huo uende kwa kasi ile ile kwa sababu mabadiliko hayo yatawezesha waandishi wa habari kuwa huru zaidi, pia kufanya kazi zao kwa weledi kwa sababu, vile vitu ambavyo tuliviona ni vikwazo, vitakuwa vimeondolewa.

“Mambo hayo yanayokwaza uhuru wa habari yakiondolewa, yatasaidia sana maendeleo ya nchi yetu kwa sababu, habari ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema mchakato huu unakwenda kwa kuwa, rais aliyepo madarakani ana dhamira njema na sekta ya habari.

Na kwamba, baada ya wadau wa habari kufanya vikao na serikali, wadau wanasubiri matunda ya vikao hivyo kwa kupelekwa mapendekezo ya wadau wa habari bungeni.

“Katika mchakato huu, tumekuwa tukishiriki kuzungumza na waziri husika ili tukubaliane katika sehemu mbalimbali ya vifungu vya sheria ya habari,” amesema Balile na kuongeza:
“Tulifanya mkutano wa mwisho Novemba ambao tulisema, sasa huu uwe mkutano wa mwisho ili sheria ya huduma za habari ipelekwe bungeni.” amesema.

Hivi karibuni, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alisema Serikali inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari ili wabunge wakiridhia utekelezaji wake ufanyike.

“Kwa sasa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria hii ili wabunge wakiridhia, tuendelee na utekelezaji wake,” amesema Msigwa.