Vita dhidi ya dawa za kulevya inakuwa ngumu baada ya watendaji waliokabidhiwa jukumu la kudhibiti biashara hii haramu kuugeuza mradi, mpango wa kutoa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini mpango wa kutoa matibabu kwa watu walioathirika na dawa za kulevya unaojulikana kama Medication Assisted Treatment (MAT) uliopaswa kuanza Agosti, mwaka huu tayari umeanza kuhujumiwa.

Chini ya mradi huo, shirika la Kimarekani lijulikanalo kama Centre for Disease Control, limetoa kiasi cha Sh bilioni 3.6, ambazo zinapaswa kutumika kuwanunulia waathirika wa dawa za kulevya dawa, maji ya kunywa na juisi, lakini watendaji wameanza kuzitumbua.

Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya inanyooshewa kidole moja kwa moja kutokana na matumizi hewa ya dola 30,000 za Marekani ndani ya wiki mbili kinyume na taratibu za mradi huu.

Mpango huu ulioundiwa kamati ya wataalamu 15 kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Taasisi ya Pangea Global AIDS Foundation; Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi; Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya; Chuo Kikuu cha Muhimbili; Hospitali ya Mwananyamala; Temeke; Mratibu wa MAT, Mratibu wa CDC na wengine, unaonekana kuingia dosari.

“Aprili 30, 2014 baadhi ya maafisa wanaosimamia mradi huu walidanganya kuwa wanakwenda kwenye semina Bagamoyo, wakajilipa dola 12,150 za Marekani (Sh milioni karibu 20) wakidai wanakwenda kupitia utekelezaji wa mradi huu. Unajiuliza wanapitia utekelezaji wa mradi ambao haujaanza?

“Mbaya zaidi, mradi huu unahitaji zaidi utaalamu wa kitabibu kwa maana ya madaktari, lakini wanaousimamia hawana utaalamu huo. La kutisha sasa, hata hiyo semina Bagamoyo haikufanyika kwani siku hiyo hiyo walikuwa na semina Morogoro, lakini fedha wamejilipa,” kilisema chanzo chetu.

Uchunguzi unaonesha kuwa wakubwa hao walijilipa tena dola 17,100 za Marekani (zaidi ya sh milioni 28) Aprili 24, mwaka huu wakidai wanapitia utekelezaji wa mradi Bagamoyo, mkutano ambao haukufanyika.

Wakati wasimamizi hawa wa mradi wakifanya ujanja huo, waathirika wa dawa za kulevya walioko katika Hospitali ya Mwananyamala hawana juisi, vikombe vya kunywea dawa za kuwaondoa kwenye tatizo la dawa za kulevya na hakuna anayejali.

Wakubwa hawa waliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu wanajilipa posho za siku mbili hadi sita, huku wakionesha kuwa kila afisa amekwenda na dereva wake Bagamoyo kwa mujibu wa nyaraka tulizonazo, wakati uhalisia hawajaenda Bagamoyo.

Taarifa za uhakika ilizozipata JAMHURI zimesema huu umekuwa utaratibu wa kawaida kwa baadhi ya maafisa wa Tume ya Kuzuia Dawa za Kulevya kutumia fedha za wafadhili kinyume na utaratibu.

“Kwa mfano, miaka mitatu iliyopita, wafadhili walitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya waathirika wa ulevi. Wodi hii imekamilika ina vitanda kama saba, lakini haitumiki kwa maana kuwa waliopaswa kuendesha mradi wametumia fedha watakavyo.

“Hata jengo lenyewe walilijenga chini ya kiwango, likawa linavuja; limekarabatiwa mara nyingi ajabu. Inasikitisha kuona kuwa kuna miradi mingi mno ya mambo ya afya, ambayo wanakaa chini wanaandika ripoti na kurejesha kwa wafadhili bila miradi kutekelezeka… huu ni ufisadi mkubwa,” kilisema chanzo chetu.

Afisa mwingine aliyeomba asitajwe jina, aliiambia JAMHURI kuwa wanaomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda aingilie kati mradi huu uliofadhiliwa na CDC kwani mbali na kuwa itakuwa aibu kwa Taifa, vijana walioathirika na dawa za kulevya ambao ni walengwa wa fedha hizi hazitawafikia kwa hali inavyoendelea.

“Mradi huu unapaswa kuanza Agosti mwaka huu hadi mwaka 2018 lakini hali inayoendelea nao utakuwa kama miradi mingine ambayo ilianza na ikaisha bila watu kufahamu iwapo ilikuwapo au la,” kilisema chanzo chetu.

Tatizo la dawa za kulevya ni kubwa hapa nchini, ambapo wanamuziki na watu kadhaa maarufu wamekamatwa nje ya nchi wakiwa na shehena za dawa za kulevya.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inapambana na wahalifu hao ikiwamo kubadili sheria, lakini inavyoelekea watu waliokabidhiwa kazi ya kudhibiti dawa za kulevya ndiyo wenye kuhujumu mchakato wa udhibiti wa dawa hizo.

JAMHURI inaendelea kufuatilia na muda si mrefu itawataja wahusika kwa majina kuhusu kiasi walichochukua, mahala walipokuwa wakati wakidai wapo Bagamoyo kwenye mkutano kumbe hawapo, kwa nia ya kuokoa maisha ya vijana waliotumbukia katika dimbwi la dawa za kulevya, ambao wafadhili wanalenga kuokoa maisha yao lakini sasa zinatafunwa na watendaji wa Serikali.

Wahusika kila JAMHURI ilipowatafuta hawakupatikana mara moja. Hata hivyo, kutokana na ukubwa wa tatizo unaoendelea, sasa gazeti limeona ni bora kuchapisha taarifa hizi za awali kuepusha madhara ya siku za usoni.

By Jamhuri