Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ametoa maagizo kwa Uongozi wa Wilaya ya Micheweni Pemba, kusimamia utatuzi wa haraka wa Mgogoro wa Msitu wa Kijiji cha Shumba Mjini.

Othman ameyasema hayo leo, huko katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni (Ukumbi wa Shame Mata) akizungumza na Viongozi wa Wilaya ya Micheweni pamoja na wananchi wa Shehia ya Shumba Mjini, ili kutafakari suluhisho la Mgogoro wa muda mrefu, kuhusu Msitu unaozunguka Jamii ya Kijiji hicho.

Amefahamisha kuwa huo ni mgogoro wa muda mrefu na unaogusa maslahi ya Kijiji hicho na kwa kuzingatia kwamba mazingira ni msingi wa maendeleo ya wote.

Amesema kuwa misitu ikitunzwa na kuheshimiwa inavyostahiki siyo tu kwamba itaimarisha mazingira bora na salama, bali hata uchumi utakuwa kupitia msitu huo.

Othman amesema kuwa Msitu ulioleta Mgogoro huo ni hazina kubwa kwa wananchi waliopo maeneo ya karibu, hivyo ulinzi na utunzaji ni jukumu la wananchi wote, na kwamba kila mmoja akitekeleza wajibu wake manufaa yatapatikana.

“Tuna Mpango mkubwa wa Kitaifa wa Zanzibar Green Legacy, unaolenga kuendeleza na kuihuisha misitu, siyo tu kwamba itufae kimazingira bali hata kiuchumi, kwani huu ukitumika vyema, maendeleo yatatamalaki bila shaka”, ameelezea Othman akibainisha mpango bora wa kuihifadhi misitu na kuepuka mizozo ya wenyewe kwa wenyewe, na hatimaye kila mmoja kunufaika na neema hiyo.

Akisisitiza faida za kuyatunza mazingira katika kujiletea maendeleo, Mhe. Othman amesema kwasasa miti ni biashara na utajiri mkubwa, bali kinachohitajika ni subra na mashirikiano, ili kufanikisha maslahi kwa wote.

Aidha Othman amemtaka Mkuu wa Wilaya kuhakikisha zoezi la uchaguzi la kuwapata viongozi linakamilika ili kuweza kusimamia msitu na kupanga shughuli za kimaendeleo.

Pamoja na msisitizo juu ya uwepo wa Kamati Mpya ya Uongozi itakayosimamia msitu huo, Mhe.Othman ametaka uwepo wa mashirikiano pamoja na kanuni za kuleta ufanisi na maendeleo, huku akiahidi kuleta Timu ya Wataalamu kutoka Idara ya Mazingira ambayo ipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ili kuwaongezea maarifa ya utunzaji.

Katika maelezo yake, Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Bi. Mgeni Khatib Yahya, amesema kwa sasa wanaelekea katika Uchaguzi wa Viongozi wa Shehia watakao simamia Msitu huo ili shughuli nyengine za kimaendeleo ziendelee kama kawaida.

Wakitoa maoni yao mbele ya Kikao hicho wananchi Bakar Khamis Khatib na Said Khamis Mwinyi, wamesema suluhisho la kudumu la Mgogoro ni kupata uongozi ambao wananchi wenyewe wameuridhia ili kusimamia uendeshaji wa Msitu huo.

Viongozi mbali mbali wamehudhuria kikao hicho akiwemo Mkuu wa Idara ya Misitu kisiwani Pemba, Bw. Masoud Bakar Masoud.

By Jamhuri