Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kumkamata Alpher Christophrer Minja mkazi wa eneo la Sanawali jijini Arusha ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa makosa ya unyang’anyi na wizi ndani ya magari ambayo yalikuwa yanaegeshwa maeneo mbalimbali ya hoteli,nyumba za kulala wageni na kwenye kumbi za starehe Manispaa ya Songea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma Marco Chilya alisema kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kuwa watu wakiwa kwenye maeneo hayo wakiwa wameegesha magari yao na kutoka kwenda kwenye hoteli au kumbi za starehe walikuwa kuibiwa mali zao walizokuwa wamezihifadhi kwenye magari yao jambo ambalo lilikuwa kero kubwa kwa wakazi wa Songea.

Alifafanua kuwa Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama walifanikiwa kupata upelelezi wa kina ambao ulisababisha kupatikana kwa mtuhumiwa ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu na kwamba baada ya mahojiano ya awali na Polisi imebainika kuwa mtuhumiwa Minja alitokea mkoani Arusha na alifika Songea mkoani Ruvuma na kufanya matukio ya unyang’anyi na wizi wa mali za raia ambazo walikuwa wamezihifadhi kwenye magari yao.

Alifafanua kuwa mtuhumiwa Minja baada ya kumuhoji kwa kina zaidi kuhusiana na matukio hayo imebainika kuwa alikuwa na wenzake watatu ambao majina yao yamehifadhiwa kwa upelelezi zaidi wanaodaiwa kuwa walikuwa wakisaidiana na Minja kufanya uhalifu kwenye maeneo ya kumbi za starehe, Hoteli, nyumba za kulala wageni na baa mjini Songea.

Kamanda wa Polisi mkoani humo amesema kuwa Minja amekamatwa kwa makosa ya unyang’ anyi na wizi ndani ya magari yaliyo kuwa yameegeshwa kwenye maeneo mbalimbali akiwa na jumla ya Laptop 10 mali ambazo zilikuwa zimeibiwa maeneo tofauti mjini Songea na kwamba mtuhumiwa Minja anatarajiwa kufikishwa mahakamani yeye pamoja na watuhumiwa wenzake watatu mara tu baada ya upelelezi kukamilika.

By Jamhuri