Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limeyapiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumatatu 19,2023 kwenda Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam huku likiwataka Wananchi kutoshiriki maandamano hayo.

Akiongea Dar es Salaam , Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amesema “Tunawatahadharisha wananchi kuhusu taarifa zinazozagaa kutoka kwa mtu mmoja kuwa kutakuwa na maandamano siku ya Jumatatu Juni 19,2023 kwenda Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam”

“Taarifa hiyo anayodai kuwa aliifikisha Polisi, tayari amejibiwa kwa kuyapiga marufuku maandamano aliyokuwa anataka kuyaratibu na kushauriwa kama ana jambo la msingi atumie vyombo mbalimbali vya kisheria anavyoweza kufika na kuwasilisha hoja zake bila maandamano ili haki zingine za wananchi za kufanya kazi wakiwa huru zisiingiliwe”

“Jeshi la Polisi linawatahadharisha Watu kutoshiriki hicho kinachodaiwa maandamano na badala yake mnahimizwa kuendelea na shughuli zenu za kiuchumi na kijamii bila hofu, hatutosita kuchukua hatua kwa mtu au kundi la watu linalotaka kuzusha taharuki kwa kuzuia Watu wengine kufanya kazi zao”

Maandamano hayo ya amani yameitishwa na kijana Mwanaharakati wa Haki za Binadamu Deusdedith Soka ambapo amenukuliwa akisema lengo la maandamano hayo ni kupinga mkataba wa Bandari kati ya Serikali ya Tanzania na DP World.

,