Hivi karibuni, nilipigiwa simu na msomaji wa makala  zangu na kuniuliza kama niliwahi kupitia moja ya makala zilizoandikwa na Profesa Kitila Mkumbo, kwenye moja ya magazeti yanayochapishwa hapa nchini. Makala hiyo ilibeba kichwa cha habari kisemacho ‘Msingi na uhalisia wa taswira ya uchapa kazi ya Lowassa’ ya Septemba 24, mwaka huu.

Nilimjibu kuwa nimeisoma. Baadaye akaniuliza je, kwanini mtu msomi tena wa hadhi ya juu anaweza akaacha shughuli zake binafsi na za kitaifa, akaamua kumzungumzia mtu binafsi (Lowassa), badala ya kuzungumzia masuala ya nchi?

Ni ukweli kabisa sikutarajia kupata swali kama hili. Nikamwomba anipe muda nitamjibu kwani kwa wakati ule sikuwa kwenye nafasi nzuri ya kumjibu. Napenda nichukue fursa hii kumjibu kwa uzito unaostahili.

Hili ni swali ambalo limekuwa likisumbua vichwa vya watu wengi ambao wamefikia kuhisi kwamba kumwandika mtu binafsi kuna maana ya kuhongwa na mhusika, kutumika, kujikomba, kutafuta ulaji, kujishusha hadhi n.k.

Katika makala husika, Profesa Mkumbo alibainisha taswira mbili zilizojengeka katika jamii kumhusu Edward Lowassa. Mosi, alisema Lowassa ni mchapa kazi, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi mgumu na kuusimamia.

Taswira ya pili alisema Lowassa si mwadilifu, na hivyo hafai kuwa kiongozi mkuu wa nchi katika kipindi hiki ambacho nchi ina njaa ya viongozi waadilifu, baada ya kuchoshwa na kashfa lukuki za ubadhirifu na ufisadi wa fedha za umma kwa takribani miongo miwili iliyopita.

Sipendi kuingia kwa undani maudhui ya  makala hiyo ya Profesa Mkumbo kwa kuwa shabaha ya makala yangu ni kumjibu msomaji aliyeuliza swali pamoja na wadau wengine wa aina yake, wanaokerwa na waandishi wanaopenda kuandika masuala ya watu binafsi.

Kwanza kabisa nampongeza msomaji huyu kwa ujasiri wake na kwa kuuliza swali zuri sana. Napenda nimjulishe kuwa kumwandika mtu binafsi ni haki yake kikatiba. Pili kusubiri kumsifia mtu hadi siku akiaga dunia ni jambo lililopitwa na wakati.

Napenda pia nimkumbushe msomaji huyu na watu wengi wa aina yake, kuwa binadamu wanatofautiana na wanyama wengine kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutambua mabaya na mazuri. Binadamu ndiye kiranja mkuu wa wanyama na viumbe vingine vyote duniani.

Isitoshe, msomi wa aina yake Profesa Mkumbo, anapozungumzia mtu binafsi, uchambuzi wake unakuwa wa kina, haki, uliofanyiwa tathmini na utafiti wa kutosha. Matokeo ya uchambuzi huo yanatoa taswira halisi ya mtu, mazingira, mwenendo, tabia ili kuwapa watu fursa ya kujifunza kutokana na uhalisia wake linganifu.

Ikumbukwe kuwa tangu enzi za ujima hadi enzi za mapinduzi ya viwanda na teknologia ya kisasa, tumefika hapa tulipo kutokana na mgawanyiko wa kazi (division of labour). Kila mtu ana taaluma yake, kipaji, ubunifu na busara kwa kadri alivyojaaliwa na Mungu wake.

Kutokana na mgawanyo huu wa kazi, wanadamu walipata fursa ya kusomea uhalisia wa viumbe vyote vinavyoishi duniani. Kuna watu waliobobea kwenye elimu ihusuyo habari zinazohusu asili na maendeleo ya binadamu (anthropologist), falsafa ya maadili (philosophy); elimu ya nafsia (psychology), elimu ya kutambua tabia kwa kuangalia(physiogromy) na kadhalika.

Pasingeandikwa makala zinazohusu watu binafsi, wanafalsafa na watu wengine mashuhuri waliowahi kutikisa dunia tangu karne ya 14 hadi 21, wasingejulikana kwa mfano, Thomas Hobbes, Karl Max, Edmund Burke, John Stuart Mill, Galileo na baadhi ya  watu mashuhuri ambao waligeuza dunia kuwa uwanja wa vita kwa mfano, Adolf Hilter (wa Ujerumani); Benito Mussolini (wa Italia); Franciscio Franco (wa Uhispania) na kadhalika.

Aidha, kutokana na kuandikwa kwa wasifu wa watu binafsi, tungali tunawakumbuka watu mashuhuri waliowahi kulitikisa Bara la Afrika katika enzi za uhai wao kama Dk. Kwame Nkrumah, Mwalimu Julius Nyerere, Patrice Lumumba, Nelson Mandela, Samora Machel, Dk. Aggrey wa Chuo cha Achimota nchini Ghana na kadhalika. Ingawa watajwa wote walishatangulia mbele ya haki lakini jamii bado inawakumbuka kupitia makala zinazoandikwa, hotuba za viongozi, na hali kadhalika majarida.

Ninachotaka kusema ni kwamba Profesa Mkumbo ametumia vizuri taaluma yake hususani usomi wake kuhabarisha jamii juu ya wasifu wa Edward Lowassa watu wamjue, wamchunguze, wamjadili, wamkosoe ili muda utakapofika wa uchaguzi mwaka 2015 wapiga kura wasipate taabu kumnadi kama atabahatika kupenya kupitia chama chake cha CCM.

Kwangu mimi namchukulia Profesa Mkumbo kama msomi aliyetumia vizuri taaluma yake. Ametoa changamoto kwa vijana wanaochipukia kwenye tasnia ya uongozi, ili waweze kumfahamu kiongozi huyu (Lowassa) na kama kuna mambo ya kujifunza kutoka kwake basi watumie fursa hii ya kusoma makala kufuatilia tabia na nyendo zake.

Sisi wachambuzi wa mambo, nasi tunajifunza kutokana na mada, makongamano, mikutano, majarida na vitabu vilivyoandikwa. Hivyo, wadau wanaopatwa na msongo wa fikra wanapaswa kuelewa kwamba kumwandika mtu binafsi si tu kunamsaidia mhusika kujitambua, bali pia kunasaidia jamii kumwelewa kiongozi wao.

Nitumie fursa hii kuwaondoa hofu wadau wote wenye fikra mgando kuwa kuzungumzia mtu binafsi hakumaanishi kwamba mwandishi amehongwa, karubuniwa, anajikomba, anajishusha au anatafuta ulaji kwa njia ya “kalamu”, la hasha. Ukweli ni kwamba tasnia ya habari ndicho chombo kikuu kinachofanya jamii itambue mazingira wanakoishi na viongozi wa aina gani wanaokaa nao.

Binafsi nimekuwa nikifuatilia kwa karibu utendaji wa Lowassa tangu kuingia kwake kwenye chama kupitia umoja wa vijana wa CCM (UVCCM). Sipendi kumung’unya maneno, Lowassa ni mchapa kazi mzuri na ni mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi mgumu na kuusimamia kama alivyodai Profesa Mkumbo.

Watanzania wanatakiwa wafike mahali wakubali kuanza kumfikiria Lowassa kuwa ni mmoja wa viongozi wanaofaa kuvaa kiatu cha Rais Kikwete mwaka 2015. Sipendi unafiki, undumilakuwili, fitina, upotoshaji, ubabaishaji, majungu na uvivu wa kufikiri ila nakiri kwa moyo wa dhati kuwa kweli Lowassa anafaa kuvaa kiatu cha Rais Kikwete mwaka 2015.

Kwa leo sitaingia kwa undani kumzungumzia Lowassa kama mtu binafsi kwa sababu shabaha ya makala yangu tangu mwanzo ni kutaka kumjibu msomaji aliyeniuliza swali juu ya mtu (profesa) kuweza kumzungumzia Lowassa ilhali kuna mambo mengi ya kitaifa aliyopaswa kuyazungumzia.

Watu wa aina yake ‘msomaji huyu’ wako wengi. Ila tu tutambue kuwa kwingineko katika mataifa ya nje, Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) na Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939-1945) ilitokana na woga wa kutowajadili watu binafsi mapema. Kama watu wa enzi hizo wangekuwa na weledi wa kuzungumzia watu binafsi, pasingetokea vita hizi za dunia.

Mwisho napenda kumuunga mkono Profesa Kitila Mkumbo kwa kusema kwamba uchambuzi wake uko sahihi. Ni kweli Lowassa ni jembe.

 

Makala hii imeandikwa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni msomaji wa JAMHURI. Anapatikana kwa namba +255 713 399 004 / +255 767 399 004

E-mail: [email protected]

By Jamhuri