Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakaribia kumaliza ujenzi wa madarasa 5,000 kuondoa zamu mbili kwa wanafunzi nchi nzima na kubakisha zamu moja.

Rais Mwinyi amesema leo Januari 9,2024 akifungua rasmi Skuli mpya ya Sekondari Tumekuja iliopo Mwembeladu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Vilevile Skuli hiyo mpya ya Tumekuja ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,755 kwa wastani wa uwiano wa wanafunzi 45 kwa darasa moja, tayari wanafunzi wameshapangwa na wiki ijayo wanatarajiwa kuanza masomo.

Aidha, amempongeza mkandarasi wa kampuni ya CRJE kwa kujenga skuli ya kisasa ambayo ina maabara tatu ya kisasa, chumba cha kompyuta, maktaba na ukumbi wa mikutano.

Rais Mwinyi amesema kuwa Serikali itaendelea kujenga maghorofa katika sekta ya elimu kwa wanafunzi kutozidi 45 kwa darasa moja .

Amesema pia, Serikali itaendelea kufanya uamuzi sahihi kwa faida ya nchi na kuyakarabati majengo ya mji mkongwe kwani ni urithi wa nchi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika elimu ni kwa juhudi za waalimu kwa kuongeza idadi ya ufaulu ikiwemo kutoka wanafunzi 2,000 hadi 6,000 skuli za msingi na matokeo ya kidato cha sita ya mwisho ufaulu wa daraja la kwanza hadi daraja la tatu kwa asilimia 90.