Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi leo amekubali barua ya kujiuzulu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), ACP Ahmed Khamis Makarani.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 2, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Charles Martin Hilary.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,hatua hiyo inakuja ikifautia maelekezo ya Rais Dkt.Mwinyi ya kuitaka ZAECA ijitathmini.

Ametoa kauli hiyo baada ya kupokea ripoti hiyo ya mwaka wa fedha 2020/21 iliyowasilishwa na CAG, Dkt.Othman Abbas Ali Ikulu jijini Zanzibar na kuonesha upotevu wa fedha katika taasisi za Serikali.

Dkt.Mwinyi amesema, kama mamlaka zinazohusika zingekuwa zinafanya kazi, isingekuwa kila mwaka yanarudiwa kutajwa mambo yale yale ya ubadhirifu.

“ZAECA lazima mjitathmini sana, hamtusaidii, sijawahi kuona Zaeca wakipeleka kesi mahakamani katika hii miaka miwili ya utawala wa Serikali hii,”amesema Dkt.Mwinyi.

Akionesha kusikitishwa kwake, Dkt.Mwinyi alisema ripoti ya mwaka jana aliipa ZAECA na kuagiza awatafute wenye matatizo, lakini mpaka sasa hajapata majibu yoyote.

“Kuna wizi mkubwa wa wazi unaotokea Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya na Mamlaka ya Mapato Zanzibar, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa,”amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Alisema kuna baadhi ya watu walihusishwa na kukiri kuchukua fedha, lakini hakuna hatua wala kusikia mtu hata mmoja aliyefikishwa mahakamani. “Kuna fedha zilizotolewa na Wizara ya Kilimo za ununuzi wa mbolea kinyume kabisa, lakini hatua hazijachukuliwa mpaka leo,”amesema.

Hata hivyo, alisema wengi hawapendi kusikia taarifa kama hizo, huku akisisitiza kuwa “lakini CAG endelea kusema ukweli, yapo mengine yana majibu, mengi hayana na huu ndio utakuwa utaratibu wetu wa kila mwaka, lazima tuweke ripoti hizi wazi na huo ndio utawala bora.

Hata hivyo, amesema ukaguzi huo unahusisha Serikali ya Awamu ya Saba na ya Nane. “Maana yake sisi tumeingia zikiwa zimeshapita robo mbili, kwa hiyo yaliyofanyika Serikali hii ilikuwa hawajaingia madarakani. Hivyo sitegemei mambo haya mwaka ujao tuyapate,”alisema.

Katika ripoti ya CAG ya vitabu sita vyenye ripoti 182 ambazo zinajumuisha Serikali Kuu, mamlaka za Serikali za mitaa na mashirika ya umma, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Afya na Kilimo zilipata hati chafu kutokana na kuonekana kuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha.

Kwa upande wa Wizara ya Afya amesema zipo zabuni zilizotolewa na kuonekana wanaidai wizara lakini kiuhalisia ni tofauti na madai yao.

Dkt.Othman Abass Ali amesema ziliagizwa baadhi ya dawa baada ya muda mfupi zilikwisha muda wake, licha ya kutumika gharama kubwa kuziagiza.

Amesema Serikali ilikadiria kupokea shilingi bilioni 24 ikiwa ni gawio kutoka katika mashirika yake mbalimbali, lakini hadi kufikia Juni, mwaka huu gawio halisi ni sh.bilioni 15.4 sawa na asilimia 64 ya makadirio.

By Jamhuri