Na Haji Mtumwa, JamhuriMedia, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa miezi mitatu bure kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa mkoa wa Kusini Unguja kufanya biashara zao bila kulipia kodi kwa halmashauri ya mkoa huo.

Ahueni hiyo ameitoa akiwa ziarani mkoani humo mara baada ya kuzindua kituo maalumu cha wafanyabiashara na wajasiriamali eneo la Kitogani kijiji cha Mtule, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja katika mwendelezo wa ziara zake za kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo nchi nzima ikiwa ni shamrashamra za mafaniko ya miaka mitatu ya uongozi wa awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi, aliitahadharisha Halmashauri ya Wilaya ya Kusini kutowawekea kodi kubwa wajasiriamali wa eneo hilo ili kuwapunguzia mzigo mkubwa wa gharama za maisha na kuwapa wepesi wa kufanyabiashara zao kwa utulivu ili kukidhi haja ya biashara zao.

Pia ameitaka Halmashauri hiyo kuyatunza na kuyadumisha kwa kuyakarabati majengo hayo yatakapoanza kuchakaa.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi amewataka wafanyabiasha waeneo hilo kudumisha usafi na kutenganisha biashara zao na maeneo ya barabara ili kuheshimu mipango ya miji iliyowekwa mkoani humo kwa kudumisha haiba ya mwonekano mzuri wa Zanzibar.

Halkadhalika, Rais Dk. Mwinyi aliitaka Halmashauri ya wilaya ya Kusini kutengeneza vyanzo zaidi vya mapato ili kuwapa uwezo wa kuendeleza miradi ya maendeleo.

Kituo hicho cha wafanyabiashara na wajasiriamali Mtule, kiligharimu shilingi Bilioni 4. 16 hadi kukamilika, kinajumuisha biashara za mbao, karakana, wachoma vyuma, gereji za magari, maduka ya bidhaa mbalimbali na wajasiriamali wa kuchora hina na piko, kina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 300 kwa kwa eneo moja.

Akiwa ziarani Kijiji cha Jozani wakati akiweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa barabara inayounganisha vijiji vinne vya Jozani – Ukongoroni – Charawe hadi Bwejuu, Rais Dk. Mwinyi aliiagiza Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi kuwalipa fidia wananchi wote waliopisha ujenzi wa barabara hiyo kabla kumalizika kwa ujenzi huo.

Rais Dk. Mwinyi, pia aliwaahidi wananchi na wakulima wa Mkoa Kusini Unguja kuwafikishia huduma za umeme mashambani ili wazalishe zaidi mboga mboga na matunda.

Alisema, Zanzibar inazaidi ya hoteli za utalii 600 zenye mahitaji mengi kutoka kwa wakulima wa ndani.

Dk. Mwinyi alisema, hakuna haja kwa Zanzibar kuagiza matunda na mboga mboga kutoka nje badala yake ameliagiza Shirika la Umeme Zanzibar, ZECO kuwafikishia huduma ya umeme wakulima wote wa Mkoa huo ili kuwapa fursa ya kutumia vyema rasilimali zilizomo kwenye vijiji vyao.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Muhammed, alipongeza uongozi wa Rais DK. Mwinyi wa kuendelea anaetatua matatizo ya wananchi wa Unguja na Pemba na kueleza mafaniko yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake yameweka alama zisizofutika kwenye historia za Wazanzibari.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano, na Uchukuzi Nadir Abdullatif Yussuf, alisifu hatua kubwa za maendeo zilizotekeleza ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi hasa kwenye miundombinu ya barabara ambapo zaidi ya kilomita 800 tayari zimetengenezwa Unguja Pemba, ujenzi wa viwanja vya ndege vya kisasa, ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani na kueleza maendelo hayo yamepita ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/ 2025.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Khadija Khamis Rajab, alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Jozani Charawe -Ukongoroni na Bwejuu ni miongoni ujenzi wa barabara ndefu za kikomita 42.5 ambapo barabara hiyo itakua na urefu wa kilomita 23.3 hadi kukamilika kwake.

Mkuu wa mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, alisema mkoa unaendelea kutawaliwa kwa amani na utulivu wa wananchi na kupongeza juhudi za Rais Mwinyi kwa kuendelea kuwaekea wananchi wa Mkoa huo eneo maalumu la wajasiriamali ili kukuza vipato vyao mbali na maendeleo mengine ya huduma za jamii iliwemo ujenzi wa barabara za kisasa zilizounganisha vijiji vya mkoa huo, huduma bora za afya zinazotolewa na hospitali yakisasa ya Kitogani, shule za kisasa na maji safi.