Na Hughes Dugilo, Hangzhou, China

Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi inayojihusisha na kuwawezesha Wafanyabiasha ya Professional Exchange Platform, (PEXPLA – TANZANIA), Jenipha Japheth, amesema kuwa wafanyabiasha wa Tanzania wanaweza kunufaika na uwepo wa ushirikiano wa kibiashara baina ya taasisi hiyo na Chemba ya Biashara ya Jinhua ya nchini China, kwa kuwafungulia milango ya kuongeza wigo wa masoko na kukopeshwa mitaji.

Akizungumza katika kikao maaluum kati ya taasisi hizo mbili, kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika Jiji la Hangzhou nchini China, Jenipha amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa baina yao yanakwenda kuongeza fursa za kibiashara kwa wafanyabiasha wa Tanzania.

“Kikao hiki ni muendelezo wa taasisi yetu ya PEXPLA katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuwainua wafanyabiasha wa dogo, wakati na wakubwa.

“Pia PEXPLA ina jukumu la kukuza mitaji ya wafanyabiasha, ambapo kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kuanza kuwadhamini wafanyabiasha hao ili waweze kuchukua mzigo kutoka kwa wazalishaji wa China kwa mkopo, na kuziuza na baadae kujisimamia wenyewe katika biashara zao” amesema Jenipha.

Ameeleza kuwa taasisi hiyo pia imeweza kutoa udhamini kwa wafanyabiasha zaidi ya 300 kwenda nchini China, kujifunza na kujionea fursa mbalimbali za kibiashara, huku ikiwakutanisha na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali katika mazungumzo ya ana kwa ana.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chemba ya Biashara ya Jinhua nchini China, anayeshughulika na mahusiano ya Biashara na Afrika, Jin Yongming ameishukuru taasisi ya PEXPLA kwa kuonesha nia ya kuongeza wigo kwa wafanyabiasha wa Tanzania, na kuahidi kuendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabiasha hao ili kufikia malengo yao.