Kufuatia mualiko wa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoloki duniani na nchi ya Vatican Papa Francis, Rais Samia Suluhu Hassan atafanya Ziara ya Kitaifa tarehe 11 hadi 12 Februari, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema lengo la ziara hii ni kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na Vatican.

Tanzania na Vatican tangiu mwaka wa 1960 zimekuwa zikishirikiana katika masuala ya elimu, afya, masuala ya amani na kiroho.

“Kanisa Katoliki linakadiriwa kumiliki zaidi ya shule za chekechea 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 245, vyuo vya ufundi 110, na vyuo vikuu 5,” inaeleza taarifa iliyotolewa na wizara huku takribani taasisi za afya 473 zikiendeshwa na Kanisa Katoliki.

Tofauti za udini hazijawafanya viongozi hawa kushindwa kukaa pamoja na kujadili maslahi ya wananchi na uendelezaji wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.