Shilingi Bilioni 72 kutekeleza miradi ya umeme mkoani humo

Zuena Msuya na Mayloyce Mpombo, Singida

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ifikapo mwaka 2024 Mkoa wa Singida hautashuka asilimia 97 ya upatikanaji wa umeme mkoani Singida.

Rais amesema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika madhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa Mkoa wa Singida yaliyofanyika katika viwanja vya Bombadia Oktoba 16, 2023 mkoani humo.

“Kwa upande wa Umeme, Naibu Waziri wa Nishati amesema hapa ikifika Desemba mwaka ujao, kama sio asilimia 100, hatutashuka asilimia 97 ya upatikanaji wa umeme ndani ya Singida”, amsema Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Singida wakati wa maadhimisho ya Miaka 60 ya kuanzishwa kwa Mkoa huo yaliyofanyika katika viwanja vya Bombadia Oktoba 16, 2023.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema Serikali imetoa shilingi Bilioni 72 kwa ajili ya kuvipatia vijiji vyote 171 ambavyo vilikuwa havijapatiwa umeme ambapo mpaka sasa Vijiji 50 vilivyobakia wakandarasi wako site wanaendelea na kazi.

Pamoja na miradi ya kusambaza umeme amesema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya kimkakati ili kuboresha uchumi wa watu wa Singida

Serikali imetoa shilingi Bilioni 7 kwa ajili ya kupelekea umeme katika maeneo ya Pembezoni mwa Miji (Peri-Urban III) katika maeneo 34.

Vilevile mradi wa kupeleka umeme kwenye Mabwawa ya umwagiliaji na migodi midogo 22 kwa gharama ya shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya kuinua uchumi wa wananchi wa mkoa huo.

“Wakazi wa Mkoa wa Singida wanakushukuru sana Rais kwa sababu umeboresha Nishati ya Umeme katika kipindi cha miaka miwili na nusu uliokaa madarakani, tunakushukuru sana kwa wema wako kwa watu wa Singida, na sisi Wizara ya Nishati tunakuahidi kuendelea kuchapa kazi na kusimamia fedha hizi ambazo umewapa watu wa Singida” , amesema Kapingatekeleza.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Singida wakati wa maadhimisho ya Miaka 60 ya kuanzishwa kwa Mkoa huo yaliyofanyika katika viwanja vya Bombadia tarehe 16 Oktoba, 2023.

Pia Bilioni 12 zimetolewa katika maeneo ya vitongoji ambapo umeme ulipita lakini haukuwafikia wananchi.

Sambamba na shilingi Bilioni 10 zimetolewa kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Singida ili kuongeza idadi ya wananchi wanaonganishwa na umeme pia kuongeza nguvu ya umeme kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Wananchi wa Mkoa wa Singida wakimshangilia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Miaka 60 ya kuanzishwa kwa Mkoa huo yaliyofanyika katika viwanja vya Bombadia tarehe 16 Oktoba, 2023.

By Jamhuri