Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, anatarajia kufanya
Ziara ya Kikazi nchini kuanzia tarehe 30 Oktoba hadi 01 Novemba 2023.


Ziara hio mbali na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Tanzania na Ujerumani, pia imelenga kwenye kukuza na
kuimarisha misingi ya biashara na uwekezaji.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikoano wa Afrika Masharikia kupitia kitengo cha mawasiliano serikalini imeeleza hayo katika taarifa iliyotolewa leo Oktoba 29, 2023.

“Ujumbe wa Rais Steinmeier utakao jumuisha viongozi wengine wa Serikali, pamoja na wawekezaji wa makampuni makubwa 12; utawasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Oktoba 2023 na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba (Mb.).” Imeeleza taarifa hiyo

Akiwa nchini, Rais Steinmeier atafanya mazungumzo rasmi na Mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam, Oktoba31, 2023.

Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao watapata fursa ya kuongea na Waandishi wa Habari kuelezea kuhusu masuala muhimu yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao.

Kadhalika, Marais hao watapata fursa ya kushiriki katika Jukwaa la Biashara, litakalohusisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo mbili, lililoandaliwa na Ubalozi wa Ujerumani kwa ushirikiano na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika Hoteli ya Hyatt Regency; ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi hao watapokea taarifa iliyojadiliwa na Jukwaa hilo.

Siku hiyo hiyo, Rais Steinmeier anatarajiwa kuonana na kuzungumza
na vijana wajasiriamali wa Kitanzania wanaojihusisha na uvumbuzi wa teknolojia
mpya hususan matumizi ya akili bandia ambao wanafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani.

Vilevile, Rais Steinmeier atatembelea Kiwanda cha Twiga
Cement Jijini Dar es Salaam kinachoendeshwa kwa ubia na Kampuni ya Scancem International ya Ujerumani.

Novemba 01 2023, Rais Stenmeier atasafiri kwenda Wilayani Songea Mkoani Ruvuma kutembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji na Shule ya Msingi ya Majimaji.

Hii ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya MajiMaji katika harakati za ukombozi dhidi
ya ukoloni wa Wajerumani.

Tanzania na Ujerumani zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu kwa muda wa miaka zaidi ya 60. Nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati hususan biashara na uwekezaji, maji, afya, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake, uhifadhi wa bioanuai, usimamizi wa fedha, utalii pamoja na malikale na utamaduni.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Tanzania imekuwa ikiuzia Ujerumani bidhaa zenye thamani ya
wastani wa Dola za Marekani milioni 42.04 kwa mwaka. Bidhaa kuu ambazo Tanzania inaiuzia Ujerumani ni pamoja na Kahawa, Tumbaku, Pamba, Asali,
Samaki, Nta na vito vya thamani.

Kadhalika, Tanzania inaagiza bidhaa kutoka Ujerumani zenye wastani wa Dola za Kimarekani milioni 237.43 kwa mwaka na bidhaa kuu zinazoagizwa kutoka Ujerumani ni Dawa, Vifaa Tiba, Mafuta (manukato, vipodozi) Magari, Vifaa na
Mashine za Umeme.

Kwa upande wa uwekezaji, Ujerumani ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini. Kwa mujibu wa TIC hadi kufikia Agosti 2023, miradi 178 ya Ujerumani yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 408.11 ilisajiliwa na kutoa fursa za ajira zipatazo 16,121.

Kwa upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imefanikiwa kusajili miradi 15 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300.00 ambayo imezalisha ajira 905.

Kampuni za Kijerumani zilizowekeza nchini zinajihusisha zaidi na sekta za kilimo, viwanda, nishati mbadala, ujenzi, utalii sanaa na utamaduni.

Kufanyika kwa ziara hii ni ushahidi tosha kuwa Diplomasia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inazidi kupaa.