Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa Tawala na Rasilimali Watu nchini kuzingatia taratibu za utumishi na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali iliyowekwa na Serikali ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Tawala na Rasilimali Watu uliofanyika katika Ukumbi wa Jenerali Mabeyo jijini Dodoma.

Mkutano huo wa mwaka uliwakutanisha Maafisa Tawala na Rasilimali Watu kutoka wizara, idara, taasisi za Serikali, taasisi zinazojitegemea pamoja na mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kujadili changamoto zinazokabili taaluma yao na kutafuta njia za kuzitatua.

Ridhiwani aliwasisitiza washiriki kuimarisha mawasiliano kati ya ofisi zao na Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora ili kurahisisha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, alibainisha matumizi ya teknolojia za mawasiliano na mifumo mbalimbali iliyobuniwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo na usimamizi wake unaochochea maboresho katika utumishi wa umma .

Alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na ujenzi na uboreshaji wa mifumo mbalimbali ya utumishi, upandishaji wa madaraja kwa watumishi wa umma, pamoja na ulipaji wa madeni yanayotokana na mishahara na stahiki za likizo.