Na wandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KABIDHI Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Frank Kanyusi amewataka wananchi na waombaji wote wa mikopo ya elimu ya juu kutosubiri dirisha la mikopo kufunguliwa ndio waanze kutuma maombi ya uhakiki RITA badala yake watume maombi mapema kwani mfumo wa kuhakiki wa vyeti upo wazi mwaka mzima.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada hafla ya kubadilishana hati za makubaliano iliyojumuisha taasisi zinazohusika na masuala ya utambuzi ambazo ni Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), CREDITINFO Tanzania Ltd ambayo ni taasisi ya uchakataji wa taarifa za waombaji mikopo katika taasisi za fedha.

“Kwa sasa, mwombaji mkopo, anatuma maombi ya uhakiki wa cheti cha kuzaliwa au cha kifo cha mzazi wake kupitia mfumo wa TEHAMA wa eRITA unaopatikana kupitia tovuti ya wakala ya www.rita.go.tz. Baada ya uhakiki kukamilika, tunampatia mwombaji NAMBA MAALUM ambayo akiingiza kwenye mfumo wa Bodi ya Mikopo – inasomeka RITA moja kwa moja,” alisema Kanyusi.

Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Frank Kanyusi kulia na kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Profesa Bill Kiwia wakionesha hati ya makubaliano wakati wa hafla ya kubadilishana hati za makubaliano iliyojumuisha taasisi zinazohusika na masuala ya utambuzi ambazo ni Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), CREDITINFO Tanzania Ltd, jana jijini Dar es Salaam.

Kanyusi alisema tangu dilisha lilipofunguliwa tarehe 1 juni 2024 wamekwisha pokea jumla ya maombi ya uhakiki 244,354 ambapo kati ya hayo, maombi 218,263 ni ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na 26,091 ya uhakiki wa vyeti vya vifo.

“Hadi kufikia leo, Wakala umeshahakiki jumla ya maombi 243,629 sawa na asilimia 99.75 ya maombi yaliyopokelewa. kati ya maombi yaliyofanyiwa uhakiki, jumla ya maombi 26,150 yalikuwa na mapungufu na waombaji walirudishiwa kwa ajili ya kufanya marekebisho na maombi 618 yalikataliwa kwani vyeti vilivyowasilishwa kwa ajili ya uhakiki havikuwa halali,” alisema Kanyusi.

Aidha Kanyusi alisema maombi 725 bado yanaendelea kuhakikiwa na zoezi linategemewa kukamilika ndani siku 1.

“Katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi inatimia sambamba na kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka mifumo ya yote ndani ya serikali kusomana ifikapo Desemba mwaka huu, RITA kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB) tumeshalitekeleza agizo hilo,” alisema Kanyusi.

Na kuongeza kuwa wakala wamejipanga kutekeleza yote yaliyomo kwenye makubaliano na HESLB sambamba na kufanya maboresho ya mfumo wa uhakiki lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi katika utendaji.

Please follow and like us:
Pin Share