Na Albano Midelo,JamhuriMedia,Ruvuma

Serikali mkoani Ruvuma imekamilisha mradi wa ujenzi wa madarasa 156 pamoja na samani zake katika shule za sekondari yaliyogharimu shilingi bilioni 3.1. 

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan mwezi Oktoba mwaka huu ilitoa fedha za kutekeleza mradi huo mkoani Ruvuma. 

“Madarasa yapo tayari kupokea wanafunzi waliochaguliwa kidato cha kwanza Januari 2023”,amesisitiza RC Thomas. 

Hata hivyo amesema hayo ni mafanikio makubwa kwa kuwa sasa katika Mkoa mzima shule zote za sekondari za Serikali zina uhakika wa kupokea wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule hizo.

Amesema hakuna kikwazo tena cha uhaba wa vyumba vya madarasa hivyo ametoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanaripoti bila kukosa. 

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 7.7 zilizojenga shule mpya za sekondari 11 mkoani Ruvuma katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022. Amesema uboreshaji wa miundombinu ya elimu umepunguza utoro na kuongeza ufaulu. 

Ametolea mfano ufaulu wa mitihani ya Taifa ya kidato cha nne mwaka 2021 Mkoa ulikuwa na ufaulu wa asilimia 90.1.

Kulingana na RC Thomas matokeo ya mitihani ya Taifa ya kidato cha sita mwaka 2022 Mkoa wa Ruvuma umefaulisha kwa asilimia 99.9. 

Hata hivyo amesema jitihada zinafanyika kuboresha ufaulu wa darasa la saba na kidato cha nne.

Please follow and like us:
Pin Share