Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewataka wananchi kutunza miradi inayotekelezwa na Serikali ili iweze kuwanufaisha katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa wito huo wakati akizindua miradi ya visima vya maji, vitalu nyumba, josho la kuogeshea mifugo na mashine ya kukamua mafuta ya alizeti wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma leo Desemba 29, 2022, inayotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizindua mradi wa katika Kijiji cha Nghambi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kukagua na kuzindua miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma leo Desemba 29, 2022.

Akizungumza na wananchi wakati wa ziara hiyo, Dkt.Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais iliamua kutenga fedha kutekeleza mradi huo kwa maeneo mbalimbali yenye ukame ikiwemo Mpwapwa ili kutatua changamoto zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Ndugu zangu mradi huu una thamani kubwa tumeona wenyewe hapa kupeleka maji zaidi ya kilometa moja na kuleta umeme hapa kwenye kisima hiki ni gharama kubwa kwa hiyo tuutunze mradi huu kwa maslahi mapana ya vijiji hivi,” amesema.

Aidha, Dkt. Jafo amezitaka Kamati za Maji za vijiji vya Ng’ambi na Mbugani ambako amezindua visima vya maji kuusimamia mradi huo ili uwe endelevu na kuleta faida kwa wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akitoa maelekezo baada ya kuzindua mradi wa josho la kuogeshea mifugo katika Kijiji cha Kazania wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kukagua na kuzindua miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma leo Desemba 29, 2022.

“Inawezekana baadae mkaongeza na tanki lingine kutoka hili moja lililopo kulingana na maelekezo ya wataalamu hivyo mtakuwa mmewezesha kupanua zaidi huduma hii na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tumetimiza jukumu letu la kuwasaidia wananchi kupambana na athari za mabadiiko ya tabianchi,” ameongeza.

Vilevile Waziri Jafo amewapongeza viongozi wilayani Mpwapwa kwa kusimamia vyema miradi hii na kusema kuwa utasaidia kujenga uchumi wa mmoja mmoja na wilaya kwa ujumla.

Katika ziara hiyo amezindua mradi wa josho katika Kijiji cha Kazania ambao utawasaidai wananchi kusaidia kuogeshea mifugo na kuwapusha na magonjwa yakiwemo kupe. Pia miradi ya visima vitatu vitakavyonufaisha wananchi zaidi ya 5000 watakapata maji safi.

Pia vitalu nyumba ambavyo wananchi kupitia vikundi wanalima mbogamboga zikiwemo nyanya pamoja na mradi wa mashine ya kukamua alizeti katika Kijiji cha Ng’ambi ambayo hukamua tani 6.5 kwa siku na kuwasaidia wananchi hao ambao awali walifuata huduma hiyo wilayani Kongwa.

Mashine ya kukamulia mafuta ya alizeti baada ya kuzinduliwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo katika kijiji cha Nghambi kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma leo Desemba 29, 2022.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mwanahamisi Ally aliahidi kushirikiana na wananchi kuutunza mradi huo ili uwe endelevu.

Amesema atashirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanaongeza mtandao wa maji kupitia visima hivyo vilivyozinduliwa kupitia Mradi wa EBARR ili huduma iwafikiwe wananchi wengi zaidi.

Ameishukuru Serikali kwa mradi huo akisema kuwa maeneo mengi ya halmashauri hiyo yamekuwa na changamoto ya maji hivyo utawanuafaisha wanachi kulima mbogamboga kupitia vitalu nyumba na kujipatia kipato

Naye Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mhe. George Malima amesema tatizo la maji sasa lililokuwa linaikabili baadhi ya vijiji katika wilaya hiyo sasa limetatuliwa kupitia mradi huo.

Mwananchi wa Kijiji cha Mbugani Elena Mpanda akiishukuru Serikali amesema sasa hivi shida ya maji ni historia kwakuwa visima hivyo vitawanufaisha tofauti na zamani walikuwa wanayafuata wilaya jirani ya Kongwa na kuyanunua shilingi 1,500 kwa dumu.

“Tunaishukuru sana Serikali kwani zamani tulikuwa tunaoga mara moja kwa wiki lakini sasa hivi maji tunayo mengi tu tunayatumia pia shughuli mbalimbali zikiwemo kupikia n ahata kujengea nyumba za kisasa,” amesema.

Katika ziara hiyo pia Dkt. Jafo alikagua maendeleo ya ujenzi wa malambo ya kuvunia maji katika Kijiji cha Kazania na Kiegea na kutoa maelekezo yakamilike kwa wakati.

By Jamhuri