Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mkurugenzi Msaidizi (Operesheni na Uratibu), Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera , Bunge na Uratibu), Luteni Kanali Selestine Masalamado amezitaka sekta kuchukua hatua stahiki kipindi cha uwepo wa hali ya El Nino katika msimu wa mvua za Vuli 2023.

Hayo ameyasema wakati wa Mkutano wa 22 wa Wadau wa Utabiri wa msimu wa Mvua za Vuli, ulioandaliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Save the Children kwa uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine Masalamado akihutubia wakati wa Mkutano wa 22 wa Wadau wa Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba, 2023) (National Climate Outlook Forum, Ncof-22 for October to December 2023 rain season) uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Giraffe, Dar es Salaam, Tarehe 22 Agosti, 2023.

“Kama alivyoeleza Kaimu Mkurugenzi Mkuu, juu ya uwepo wa hali ya El Nino, napenda kutoa msisitizo kuwa, katika majadiliano haya, ni vyema kujikita katika kufanya tathmini na kuainisha athari zinazoweza kujitokeza katika msimu huu na kuchukua hatua stahiki”.Alisisitiza Luteni Kanali Masalamado. Aidha, alitoa wito kwa wadau kutoka sekta mbalimbali kushirikiana na TMA ili kufanikisha upatikanaji wa taarifa za kisekta.

Awali, Luteni Kanali Masalamado aliipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali katika shughuli zao za utoaji wa huduma za hali ya hewa ambazo ni pamoja na utabiri wa misimu ya mvua. Alisema ushirikiano unaofanyika ni mfano wa kuigwa na unafaa kuendelea hasa katika kipindi hiki ambapo nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dr. Ladislaus Chang’a akizungumza kuhusu masuala ya utabiri wa hali ya hewa wakati wa Mkutano wa 22 wa Wadau wa Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba, 2023) (National Climate Outlook Forum, Ncof-22 for October to December 2023 rain season) uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Giraffe, Dar es Salaam, Tarehe 22 Agosti, 2023.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza kuwa ni muhimu izingatiwe kuwa katika msimu huu wa Vuli, 2023 mifumo ya hali ya hewa inaonesha uwepo wa hali ya El Nino ambayo ilianza kujitokeza mapema mwezi Juni, 2023 na imeendelea kuimarika.Alisema“Mkutano huu ni muhimu sana kwa wadau wa hali ya hewa kupata fursa ya kujifunza kwa undani na kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta mbalimbali na hivyo kuendelea kuboresha na kuongeza tija”


Mkurugenzi wa Programu kutoka Shirika la Save the Children Bw. Snatoli Rugaimukamu akiwasilisha salamu za shirika hilo wakati wa mkutano huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Programu kutoka Shirika la Save the Children, Bw. Anatoli Rugaimukamu, amesema kikao hiki kinatoa mwelekeo wa jinsi ya kujipanga kukabiliana na maafa hususani kwa waathirika wakubwa ambao ni watoto.

TMA inatarajia kutoa rasmi utabiri wa Msimu wa Vuli 2023 utakaojumuisha maoni na ushauri wa wadau kuhusiana na athari (hasi au chanya) zinazoweza kutokea kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa katika msimu huu.


Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa 22 wa Wadau wa Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba, 2023) wakifuatiliwa mawasilisho wakati wa mkutano huo.

By Jamhuri