Na Albano Midelo, JamhuriSongea

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imedhamiria kuona idadi ya faru Weusi inaongezeka kwa asilimia tano kila mwaka.

Mratibu wa Faru kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Philibert Ngoti amesema hadi kufikia Aprili 2023,idadi ya faru nchini ilifikia 238 hivyo kuvuka lengo la mpango wa Taifa wa kuongeza faru Weusi ambalo lilikuwa ni faru 205 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2023.

“Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1970 hadi 1980 Tanzania ilikuwa na faru Weusi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa nchini waliofikia 10,000 hivyo Tanzania ilijulikana kama nchi yenye faru wengi barani Afrika’’,alisema Ngoti.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza baada ya kuzindua Mkakati wa Utalii Mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea

Hata hivyo alisema mwanzoni mwa miaka ya 1980 hadi 1990 idadi ya faru ilipungua na kuwa chini ya 100,kutokana na uwindaji haramu na kwamba upungufu wa faru pia ulitokea katika nchi zote zenye faru barani Afrika.

Amesema kutokana na hali hiyo faru Weusi waliwekwa kwenye kundi la Wanyama walio hatarini kutoweka duniani na kwamba mwaka 1993 serikali ya Tanzania ilikuja na toleo la kwanza la mpango wa Taifa wa miaka mitano la uhifadhi wa faru Weusi.

Mratibu huyo wa Faru Taifa amesisitiza kuwa ,Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuunda sera na mipango ya usimamizi na uhifadhi wa faru Weusi na kwamba mpango huo unaoanzia mwaka 2019 hadi 2023 hivi upo katika toleo la nne.

Amebainisha zaidi kuwa Mpango wa Taifa wa Uhifadhi na Usimamizi wa Faru Weusi wa mwaka 2019 hadi 2023 unahimiza kuja na mazao ya utalii kwa kutumia faru Weusi waliopo.

Kulingana na Mratibu huyo,kuna aina tano za faru duniani kati ya hizo faru weupe wapo wa aina tatu ambao wanapatikana katika bara la Asia na aina mbili za faru Weusi wanapatikana katika bara la Afrika.

“Nchini kwetu tuna faru Weusi pekee ambao wamegawanyika katika aina mbili ambazo ni faru Weusi wa mashariki na faru Weusi wa kusini kati,faru mweusi aina ya kusini kati anapatikana kusini mwa Tanzania ukiwemo Mkoa wa Ruvuma’,alisema Ngoti.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaagiza wadau wa utalii kuhakikisha wanaendelea kuwahifadhi Wanyama faru ambao wapo katika hatari ya kutoweka kutokana na vitendo vya majangili na watu wote wenye nia ovu dhidi ya Wanyama hao.

Amesisitiza kuboreshwa kwa uhifadhi wa Wanyama hao kutasaidia kuendelea kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwepo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Ametoa rai kwa wadau wa maendeleo wakiwemo WWF,GIZ na PALMS kuona umuhimu wa kuanzishwa bustani ya faru katika wilaya ya Namtumbo kwa kuwa tayari eneo ambalo faru Weusi waliwahi kuishi limeainishwa.

Faru mweusi ni mnyama mwenye pembe mbili ,ana uzito wa kilo kati ya 700 hadi 1,500,urefu mita 3.5,ni mnyama mwenye hasira na huwa hatabiriki.

Ni vema mataifa yote ambayo yamebakiwa na faru kushirikiana kuwahifadhi na kuwalinda wanyama hao adimu ambao wapo katika hatari ya kutoweka katika uso wa Dunia.

By Jamhuri