Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe
Serikali imeahidi kuendelea kuiwezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi(Osha), vitendea kazi ili kuleta ufanisi katika shughuli zake.
Ahadi imetolewa na Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, wakati akifunga maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi,yanayofanyika viwanja vya shule ya Mjimwema mkoani Njombe
Waziri Sangu amesema Serikali inafanya hivyo kwa kuwa OSHA ni taasisi muhimu katika kuleta ufanisi kwa wafanyakazi.
“Hivyo Serikali ina wajibu kuiwezesha OSHA vitendea kazi vyote muhimu ikiwemo magari na vifaa vya ukaguzi,”amesema Waziri Sangu.
Hata hivyo amesema hadi sasa Serikali imeipatia OSHA magari 50 na vifaa vya ukaguzi vyenye thamani ya Shilingi bilioni 7.
Katika maadhimisho hayo pia Waziri Sangu ameiagiza OSHA, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii( NSSF), kuhakikisha zinawabana waajiri ili wajisajili na kulipa madeni katika mifuko hiyo.
Akielezea OSHA ,amesema licha ya kuwepo kwa waajiri 200,000 lakini waliofikiwa na OSHA hawazidi 100,000.
“Suala la kujisajili OSHA ni takwa la kisheria na sio hiari hivyo kila mwajiri anapaswa kujisajili huko,”amesema.
Kwa upande wa WCF,amesema kuna sekta binafsi hawataki kuwasajili wafanyakazi wao katika mfuko huo na kutoa siku 90 kufanya hivyo kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi(TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amesema kuwa kama kuna wafanyakazi ambao hawalioni bango la OSHA katika maeneo yao ya kazini vyema wakatoa taarifa ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Hawa OSHA hutoa mabango katika maeneo ya kazi ambayo wameshayasajili, hivyo kama hulioni ofisini kwako toa taarifa ili tuweze kuchukua hatua,”amesema Nyamhokya.
Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usalama na afya Mahala pa Kazi(OSHA), Khadija Mwenda, amesema katika maadhimisho hayo wameweza kuwafikia wajasiriamali 6101 na maofisa usafirishaji 300 na kuwapa vifaa kinga ikiwa kuhamasisha uwepo wa mazingira salama.
Katika ahadi yake,Khadija amesema wataendelea kuhimiza,kushauri kuhusiana na masuala ya afya na usalama mahali pa kazi kwani kutasidia kuokoa fedha za serikali na kuleta uvumilivu katika mifuko ya wafanyakazi.




