Serikali imeahidi kufanya marekebisho makubwa yanayohitajika katika uwanja wa Benjamin Mkapa ili kukidhi viwango vya kimataifa vinavyohitajika katika michuano ya Africa Super League ambayo Klabu ya Simba ndio mwakalishi wa ukanda wa Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa Februari 16, 2023 jijini Dar es Salaam na Saidi Yakubu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo alipokutana na uongozi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) ambao unaongozwa na Mohammad Sidat,Mkuu wa Kitengo cha ufundi alieambatana na wataalaam kutoka Italia waliokodiwa na Shirikisho hilo.

Bwana Yakubu alieleza kuwa maeneo yote yaliyoainishwa yatafanyiwa kazi kabla ya ziara nyingine ya ukaguzi itakayofanywa na CAF.

Aidha Yakubu pia aliwaeleza viongozi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inakusudia kujenga viwanja vingine vya michezo na watategemea sana miongozo ya kitaalamu toka FIFA na CAF.

Kwa upande wao,ujumbe huo wa CAF waliarifu kuhusu hatua za haraka zinazotakiwa kufanywa ili uwanja uendelee kutumika kimataifa na kupongeza maendeleo ya soka nchini.

Uongozi wa klabu ya Simba uliandaa hafla hiyo ya chakula cha jioni iliyohudhuriwa pia na Naibu Spika,Mussa Azzan Zungu kwa nia ya kufanya tathmini baada ya ukaguzi kufanyika.

By Jamhuri