Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
SERIKALI imeendelea kuimarisha mifumo ya uratibu, kujiandaa na kukabiliana na maafa ili kuhakikisha misaada ya kibinadamu inayotolewa inawafikia walengwa kwa wakati, ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Hayo yameelezwa leo tarehe 02 Juni, 2026 na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Kanali Selestine Masalamado, wakati wa ufunguzi wa warsha ya zoezi la uigaji la uratibu wa utoaji wa misaada ya kibinadamu na usafirishaji wakati wa dharura, mkoani Morogoro.
Amesema utoaji wa misaada ya kibinadamu na usafirishaji wa dharura ni nguzo muhimu zinazowezesha kuokoa maisha ya wananchi walioathiriwa na maafa, kupunguza mateso ya waathirika na kuharakisha urejeshaji wa hali za kawaida katika maeneo yaliyoathirika.
“Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya uratibu, kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha misaada inawafikia walengwa kwa wakati, ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya utoaji wa huduma za kibinadamu,” amesema.
Vilevile, amelishukuru Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), washirika wote waliohusika katika utekelezaji wa Mradi wa Field-Based Preparedness Project (FBPP), ambapo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mradi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uwezo wa taifa katika sekta ya utoaji wa misaada ya kibinadamu na usafirishaji.
Amesema Tanzania imefanikiwa kuanzisha Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Uratibu wa utoaji wa misaada ya kibinadamu na usafirishaji wa dharura mwezi Julai 2025, ambacho kimekuwa jukwaa muhimu la uratibu na ushirikiano baina ya taasisi za serikali na wadau wa kibinadamu.
“Zoezi hili la uigaji limeandaliwa kama jukwaa la kitaifa la kujifunza, kupima na kuboresha mifumo yetu ya uratibu wa shughuli za usafirishaji na utoaji wa misaada ya kibinadamu.”alieleza
Katika hatua nyingine, Kanali Masalamado amesisitiza umuhimu wa kuendelea kujumuisha masuala ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa tabianchi katika mipango na shughuli za usafirishaji wa misaada ya kibinadamu ili kuhakikisha kuwa hatua tunazochukua leo hazisababishi changamoto mpya kwa vizazi vijavyo.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bi. Christine Mendese amesema, Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto za maafa kwa kutoa misaada ya kibinadamu ili kuwa na jamii stahimilivu dhidi ya majanga hususan katika kuzuia na kukabiliana na majanga mbalimbali.
Kwa upande wake Mratibu wa Maafa mkoa wa Pwani Bi.Roseline ameshukuru uwepo wa warsha hiyo itakayosaidia kuongeza uelewa katika masuala la utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa maafa.
“Warsha hii imekuja wakati sahihi kwa kuzingatia mikoa ndiyo inaratibu masuala ya maafa kwa ngazi za Halmashauri zetu, tunashukuru kwa niaba ya ofisi ya mkoa kwa namna wadau mlivyoleta warsha hii na kutujengea uwezo, hii itaongeza tija katika masuala ya logistics wakati wa maafa na kusaidia kuwa na mwelekeo sahihi na kuepuka changamoto wakati wa kutekeleza majukumu ya logistics wakati wa maafa,” alisema Kimaro.










