Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanisha vipaumbele vyake vya mwaka 2023 kwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao nchini.
 
Vipaombele hivyo vimeainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipokutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Januari, 2023.
 
“Misimamo ya Tanzania ni kuwa hatufungamani na upande wowote lakini pia Tanzania ni muumini wa uendelezaji wa ushirikiano wa kimataifa na kikanda. Tumeelezana vipaumbele vya Serikali hususani utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi na kuona ni jinsi gani mabalozi wanaweza kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya pande zote,” amesema Dkt. Tax
 
Dkt. Tax aliongeza kuwa amesisitiza umuhimu wa maboresho yanayofanywa na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuboresha shughuli za kiuchumi, ambapo Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na wameridhika na maboresho yanayofanywa na Serikali na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za kipaumbele zaidi ambazo Tanzania imeziainisha.
 
Kwa upande wake kiongozi wa Mabalozi nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini, Dkt. Ahmada El Badaoui Mohamed ameishukuru Serikali kwa kuainisha vipaumbele vyake kwa mwaka 2023 na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa inafika malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka 2023.
 
“Kwa niaba ya Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya Kimataifa, napenda kuahidi kuwa tutaendelea kushirikiana na wizara na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha inafikia viapombele na malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka 2023,” alisema Balozi El Badaoui Mohamed.
 
Mkutano huo ulilenga kufahamiana, kukumbushana na kutoa mwelekeo wa Serikali ya Tanzania katika masuala ya Diplomasia na mahusiano yake na nchi na taasisi mbalimbali kwa wana jumuiya hao wa kidiplomasia wanaowakilisha hapa nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na waheshimiwa Mabalozi kutoka nchi za Asia na Australasia wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimatifa wanaowakilisha mashirika yao hapa nchini
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam wanaonekana mbele katika picha
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam hawapo pichani

By Jamhuri