Na Mwandishi Wetu,Dodoma

Serikali imesema itaendelea na juhudi za kupambana na magugu maji katika Ziwa Victoria ili kudhibiti uhabirifu wa mazingira na athari zitokanazo na uharibifu huo nchini.

Hayo yalielezwa bungeni jana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Kabula Enock Shitobela aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuondoa magugu yanayosababisha uchafuzi katika Ziwa Victoria.

Khamis alisema ili kudhibiti magugu maji yasiendelee kuleta athari katika ziwa hilo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Alitaja hatua hizo kuwa ni kutekeleza Mradi wa Hifadhi ya Mazingira katika Ziwa Viktoria (Lake Victoria Environmental Management Project – LVEMP) ambao pamoja na mambo mengine ulitekeleza shughuli zilizolenga kudhibiti magugu maji kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo za kibaiolojia.

Pamoja na hatua hiyo amebainisha kuwa Serikali inatoa elimu na kuwajengea uwezo wananchi wanaoishi karibu na ziwa kuhusu namna ya kujitolea katika kazi za kutokomeza magugu maji kila yanapojitokeza ziwani.

Aidha, Naibu Waziri alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa na inatekeleza Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Kukabiliana na Viumbe Vamizi wa mwaka 2019-2029 ambao unatoa mwongozo wa namna ya kuzuia kuingia na kuenea kwa viumbe vamizi na pia una mipango endelevu ya kushughulikia viumbe vamizi waliopo na wale wale wanaoweza kuingia.

”Mheshimiwa Spika Serikali itaendelea na juhudi hizi za kupambana na magugu maji katika Ziwa Victoria ili kudhibiti uhabirifu wa mazingira na athari zitokanazo na uharibifu huo nchini,” alisisitiza Naibu Waziri Khamis.

By Jamhuri