Serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2023/24 kwa ajili ya utekelezaji mkubwa wa miradi ya umwagiliaji katika bonde la Mto Ruvuma, Ruhuhu na Litumbandyosi mkoani Ruvuma.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo,Anthony Mavunde katika ziara ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango mkoani Ruvuma.

Amesema, serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya umwagiliaji mkoani Ruvuma ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/24 Serikali itafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na ujenzi wa miumbombinu ya Umwagiliaji katika Bonde la Mto Ruvuma wenye jumla ya hekta 26,066, Mto Ruhuhu wenye hekta 3,700 na Litumbandyosi hekta 900,”amesema Mavunde na kuongeza

“Pia itajumuisha uchimbaji wa mabwawa makubwa matano na ukarabati wa skimu za umwagiliaji katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma.”amesema.

Mavunde, amesema Mkoa wa Ruvuma umezalisha zaidi ya tani milioni 1 ya mahindi,ni mkoa ambao serikali itawekeza kiasi kikubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

Amesema, pia serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa soko la uhakika wa mazao ya wakulima ambapo tayari vituo 17 vya Wakala wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) vimefunguliwa mkoani humo.

“Mbolea ya ruzuku itaendelea kutolewa kama msimu uliopita,na kwasasa tumesajili vituo vingi zaidi vya mauzo ya mbolea ili wakulima wasifuate mbolea umbali mrefu kama ilivyokuwa msimu uliopita.” amesema.

By Jamhuri