Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imeipongeza Taasisi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa juhudi zake za kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wenye ulemavu, ikisema hatua hiyo inaendelea kufungua fursa za ajira na kuwawezesha vijana wengi kuchangia maendeleo ya taifa kupitia ujuzi wa kazi.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 jijini Dodoma, ambapo Serikali ilivutiwa na uwezo wa kijana mwenye ulemavu aitwaye Joseph aliyepata mafunzo kupitia VETA na kubobea katika usanifu wa majengo kwa kutumia mifumo ya kompyuta.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema mafanikio ya Joseph ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa na VETA katika kuwajengea vijana stadi za maisha na kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
Amesema alipata nafasi ya kuzungumza na kijana huyo wakati wa kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kujionea kiwango kikubwa cha ubunifu na utaalamu alionao katika kazi za usanifu wa majengo.
“Nimezungumza naye kwa kina na nimejiridhisha kuwa ana uwezo mkubwa sana,huyu ni mfano wa vipaji vilivyopo nchini ambavyo vinahitaji kuibuliwa na kuendelezwa,naipongeza VETA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwafikia vijana hawa na kuwapa stadi za maisha,” amesema Prof. Shemdoe.
Kutokana na umahiri huo, Prof. Shemdoe amemuelekeza Katibu Mkuu wa Utumishi kuhakikisha Joseph anatafutiwa ufadhili wa masomo ili aendelee kujiendeleza katika taaluma ya teknolojia na usanifu wa majengo.
Aidha, amesema ameelezwa kuwa kijana huyo kwa sasa anafanya kazi kupitia VETA kwa mkataba hivyo akaagiza kuanza kwa mchakato wa kumpatia ajira ya kudumu serikalini kutokana na uwezo aliouonesha.
Katika hatua nyingine, Serikali imeagiza kuchukuliwa hatua dhidi ya maafisa rasilimali watu watakaobainika kusababisha watumishi wa umma kushindwa kupanda madaraja kwa uzembe licha ya kutimiza vigezo vinavyotakiwa.
Prof. Shemdoe amesema baadhi ya maafisa hao wamekuwa wakisababisha ucheleweshaji wa haki za watumishi kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati, hali inayolazimu baadhi ya watumishi kusafiri kutoka maeneo ya mbali kufuatilia stahiki zao.
Prof. Shemdoe amebainisha kuwa hata yeye aliwahi kukumbwa na changamoto ya kucheleweshewa kupanda cheo kwa mwaka mmoja kutokana na kutokukamilishwa kwa taratibu muhimu za kiutumishi na afisa husika.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza kufanyika tathmini ya maafisa rasilimali watu wakuu waliosababisha watumishi kushindwa kupanda madaraja katika mwaka wa fedha 2025/2026 ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.
“Mimi pia ni mhanga,ninachozungumza nakielewa,hivyo nawaagiza wakuu wa Taasisi na maafisa rasilimali watu wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za watumishi badala ya kuwa chanzo cha malalamiko yanayoweza kuepukika,”amesema na kuongeza,
“Jaribuni kuvaa viatu vya watumishi hawa,Wapo wanaotoka pembezoni mwa nchi na kutumia muda na fedha nyingi kufuatilia stahiki zao hapa Dodoma ilhali wamekidhi masharti yote,hii si haki na haipaswi kuendelea kuvumiliwa,” amesema.
Amesisitiza kuwa watumishi wanaotimiza vigezo vya kupandishwa madaraja hawapaswi kunyimwa haki hiyo kwa sababu ya uzembe wa mtu mmoja au urasimu usio wa lazima.
Sambamba na hilo, ameagiza kufanyika sensa maalum ya mifumo yote ya TEHAMA inayotumika serikalini ili kubaini uwezo wake na kuhakikisha mifumo hiyo inaunganishwa na kuwasiliana kwa ufanisi.
Amesema baadhi ya mifumo iliyobuniwa kwa gharama kubwa imekuwa ikifanya kazi kwa kujitegemea bila kusomana, jambo linalosababisha usumbufu katika utoaji wa huduma na kupunguza ufanisi wa utendaji kazi.
Kutokana na hali hiyo, alimuelekeza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kusimamia tathmini ya mifumo yote ya kidijitali iliyopo serikalini na kuhakikisha inaunganishwa ili kuongeza uwazi, ufanisi na kasi ya utoaji huduma kwa wananchi.
Aidha, amewataka waajiri wote kutenga fedha za ushiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora kupitia maonesho hayo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Umoja wa Afrika la kuadhimisha Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika.
Amesema maadhimisho hayo yanalenga kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya taifa, kuhamasisha ubunifu katika utoaji wa huduma na kupata mrejesho kutoka kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi za umma.
Mkomi ameongeza kuwa maonesho ya mwaka huu yameonesha namna Taasisi za umma zinavyoendelea kutumia ubunifu, teknolojia na maendeleo ya rasilimali watu kuboresha huduma kwa wananchi, huku mafanikio ya VETA yakitajwa kuwa mfano wa uwekezaji unaozalisha matokeo chanya kwa vijana na taifa kwa ujumla.









