Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Songea

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetenga Zaidi ya shilingi bilioni 2.238  kutekeleza miradi mitano ya maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) Mhandisi Patrick Kibasa  amesema hadi sasa fedha ambazo zimeidhinishwa kutekeleza miradi hiyo ni Zaidi ya shilingi bilioni 1.37.

Amesema kati ya fedha hizo,serikali imetoa Zaidi ya shilingi bilioni 145 kutekeleza mradi wa maji wa kimkakati wa miji 28 katika mji wa Songea na kwamba mradi huo umeanza kutekelezwa tangu Januari 2024.

Ameitaja miradi mingine inayotekelezwa katika Manispaa ya Songea kuwa ni ujenzi wa mradi wa maji katika kata ya Subira ambao umeidhinishiwa Zaidi ya shilingi bilioni 1.17 na kwamba mradi umetekelezwa kwa Zaidi ya asilimia 40.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa SOUWASA,serikali imeidhinisha Zaidi ya shilingi milioni 322 kutekeleza mradi wa maboresho ya uzalishaji maji katika mji wa Mbinga ambapo mradi umetelezwa kwa asilimia 100.

Ameitaja miradi mingine ambayo imekamilika kwa asilimia 100 ni mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji safi katika mji wa Tunduru ambapo serikali imeidhinisha Zaidi ya shilingi milioni 355 na mradi wa maji eneo la viwanda kata ya Lilambo Manispaa ya Songea ambapo serikali imeidhinisha Zaidi ya shilingi milioni 415.

“Katika Manispaa ya Songea hadi kufikia mwaka 2023,wakazi 260,733 wanapata huduma ya maji sawa na asilimia 88.0,mahitaji ya Maji katika Manispaa ya Songea ni wastani lita milioni 20.593 kwa siku’’,alisisitiza Mhandisi Kibasa.

Hata hivyo amesema mwaka 2023 katika maeneo ya Manispaa ya Songea,uzalishaji wa maji ghafi ni wastani wa mita za ujazo 9,170 kwa siku na kwamba jumla ya maunganisho ya maji safi ni 22,465 ambapo upatikanaji wa huduma ya maji safi ni saa 23.15 kwa siku.

Mary Luoga na Joseph Komba ni wakazi wa Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea ,wanamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji katika kata hiyo ambapo wananchi wananufaika kwa kupata maji safi na salama.

Diwani wa Kata ya Subira Manispaa ya Songea Mheshimiwa John Ngonyani kwa niaba ya wananchi wa Kata hiyo amesema tangu uhuru kata hiyo haijawahi kupata maji safi na salama ya bomba ambapo serikali ya awamu ya Sita imetoa fedha za kutekeleza mradi wa maji ambao unakwenda kupunguza kero ya maji.

Manispaa ya Songea ina wakazi wapatao 286,285 kwa mujibu wa takwimu za sensa  ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Moja ya miradi ya maji ya SOUWASA inayotelezwa katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma 

Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA Mhandisi Patrick Kibasa