Na WAF – Dar es Salaam

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amezitaka shule zote za msingi na sekondari nchini kuwepo na mazoezi ya viungo kwa wanafunzi ikiwepo kukimbia, mchakamchaka, kutembea na kucheza ngoma au mpira kwa lengo la kupunguza Magonjwa Yasiyo ambukiza.

Hayyo yamesemwa wakati akizindua Mkutano wa Kikundi cha Utafiti wa Magonjwa ya Kisukari na magonjwa Yasiyo ambukiza kwa ukanda wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam.

“Nitoe wito kwa Watanzania mazoezi sio lazima uende ‘Gym’ wala sio lazima ukimbie lakini ukipata hata dakika angalau 30 kwa siku kwa kutembea na ukatoka jasho inatosha.” amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema lengo la kuzindua kikundi hicho ni kujadili kwa pamoja jinsi ya kuboresha huduma kwa watu wenye ugonjwa wa Kisukari na magonjwa yasiyoambukiza katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Kikundi hiki ni cha Wataalamu mbalimbali katika sekta ya afya hususan madaktari bingwa kutoka nchi za Afrika na nje ya Afrika.” amesema Waziri Ummy

Sambamba na hilo, Waziri Ummy amesema kwa sasa nchi ya Tanzania kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, magonjwa ya Moyo, shinikizo la damu na Saratani.

“Mkutano huu ambao umeandaliwa unalengo pia la kushauri Serikali ni jinsi gani tutaweza kuimarisha na kuboresha huduma kwa wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari.” amesema Waziri Ummy

Pia, Waziri Ummy amebainisha kuwa Takwimu za mwaka 2012 zinaonesha katika kila watu 100 watu 9 wana ugonjwa wa Kisukari ambapo mwaka huu Serikali itafanya tafiti nyingine kwa kuwa inaonekana kuna wagonjwa wengi wa Kisukari nchini.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari kwa kuhamasiha ufanyaji wa mazoezi.

By Jamhuri