Siasa za mauaji zisipewe nafasi

Tumeshitushwa na aina ya kifo cha Alphonce Mawazo – Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Geita.

Amekutwa na mauti kwa kile kinachodaiwa kuuawa kinyama kwa kushambuliwa na silaha za jadi ikiwamo kukata kichwa kwa shoka.

Baadhi ya vyombo vya habari na mitandao, vinaripoti kwamba ulikuwa ni mpango wa kulipa kisasi dhidi yake wauaji wanadaiwa kumteka Mawazo aliyekuwa Katoro kwenye Kikao cha ndani kwa maandalizi ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Ludete, uliofanyika juzi Jumapili. Kikao kilifanyika Ukumbi wa Makungu uliopo Mtaa wa CCM mjini Katoro.

Taarifa zaidi zinapasha ndani ya kikao hicho kulikuwa na mtu waliyehisi kuwa ni mamluki na baada ya kumuhoji, wajumbe walianza kumpiga na ndipo kikundi cha vijana waliokuwa nje kilipoingia na kuanza mapambano.

Baada ya kuona hivyo, Mawazo alitoka na kuchukua pikipiki ili kutoroka eneo hilo, lakini alifuatwa na gari moja na walipomfikia walimkamata na kumshambulia.

Wakati Kamanda wa Polisi Mkoa, Latson Mponjoli akishindwa kutoa taarifa kwa wakati akisema anafuatilia, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk. Adamu Sijaona alithibitisha kifo cha mwanasiasa huyo.

Awali alisema walimpokea majeruhi saa 9:00 alasiri akiwa katika hali mbaya na alikuwa hajitambui kutokana na majeraha makubwa katikati ya kichwa.

Alisema Mawazo alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi wakati madaktari wa hospitali hiyo wakijaribu kuokoa maisha yake.

Tunaungana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuvitaka vyombo vya dola kutoa taarifa kamili ya wahusika wa unyama huu.

Tunasema kwamba Tanzania haijafikia siasa za aina hiyo za watu kujeruhiana kiasi cha kusababisha kifo katika ardhi ya nchi ambayo inapigiwa mfano wa kuigwa.

Kilichofanywa na wauaji hao, si kwamba wamevunja amri ya tano kati ya 10 za Mungu inayosema kwa neno moja tu: “Usiue”, bali pia wamevunja Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2005 inayozungumzia haki ya kuishi.

Ibara hiyo, inasema: “Kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.”

Kisheria, watuhumiwa watakuwa wametenda kosa la jinai, miongoni mwa makosa yaliyoainishwa katika sehemu ya 25 ya kitabu cha kanuni ya adhabu.

Kama waliua kwa makusudi au kwa bahati mbaya itakuwa ni kazi ya mahakama si gazeti la JAMHURI kufafanua, lakini ili kukomesha tabia ya kukatisha maisha ya watu ovyo kama hii, vyombo husika vichukue stahiki kwa mujibu wa sheria.

Ndiyo maana sisi JAMHURI tunasema, siasa za mauaji zisipewe nafasi Tanzania. Hatujazoea. Na hatuzitaki.