Spika amtaja rais ajaye

Job Ndugai-1Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, amesema kuwa nchi kwa sasa inahitaji rais jasiri atakayeweza kuwa tayari kusimama kwa ajili ya nchi yake na watu wake.
Ndugai aliyasema hayo katika mahojiano maalum na Gazeti la JAMHURI yaliyofanyika Dodoma alikobainisha kuwa anatamani kuona Tanzania ikipata rais mwenye moyo wa kufanya analoamini.
 “Ningependa tupate rais mwenye courage (ujasiri). Hii ni kutokana na nchi kuwa na changamoto kubwa ya umaskini,” anasema Ndugai.


Anasema kwamba kuongoza Tanzania kwa sasa ni ngumu kutokana na changamoto nyingi hususani umasikini, hivyo nchi inahitaji rais atakayekuwa tayari kutumia rasilimali chache zilizopo kuboresha maisha ya Watanzania.
Alipoulizwa ni nani hasa anayeonekana kuwa na sifa hizo kati ya wale wanaotajwa, mara moja Ndugai akajibu, “Kwa sasa siwezi kusema lolote zaidi, ila naamini CCM itateua mtu anayestahili.”


Katika hatua nyingine, Ndugai alifafanua sababu zake za kutoonekana akiendesha vikao vya Bunge kwa muda mrefu hasa kukiwa na taarifa kwamba amezuiwa. “Binafsi sijawekewa zuio. Nilikuwa jimboni kwa wapigakura wangu ambao ndiyo waajiri wangu.”
Pia alibainisha kuwa suala la Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuonekana mara kwa mara akiendesha vikao vya Bunge ni kazi yake anayotakiwa kuifanya siku zote naye ni msaidizi tu, pale anapohitajika kufanya hivyo na si vinginevyo.
Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa anaumwa na kwamba huenda nje ya nchi kutibiwa, pia akajibu, “Hata mimi nazisikia taarifa hizi, lakini sina tatizo lolote na ni mzima wa afya njema.”


Anasema anaamini kuwa utendaji wake wa kazi umekuwa ni wa mafanikio makubwa kwa kuendesha Bunge la 10 ambalo limeboreka kimtazamo katika mabadiliko yake kutokana na wabunge kupewa nafasi kubwa ya kujadili mambo tofauti na ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.
“Watu wanaongea kwa uwazi zaidi, wabunge wamekuwa huru zaidi, wanasema bila woga wowote ule, zamani ilikuwa vigumu kuwakuta wabunge wanajadili kama ilivyo sasa,” anasema Ndugai na kuongeza: “Watu walikuwa wanatoa majina wakiona hoja ni ngumu. Lakini hivi sasa mbunge anakomaa mpaka anafikia hatua ya kuhatarisha ajira ya kiongozi bila woga wowote. Kwa hiyo, tumesonga mbele.”  


Kadhalika, JAMHURI ilipotaka kufahamu iwapo atagombea nafasi ya uspika baada ya Uchaguzi Mkuu ujao, lakini akasema, “Natamani kubaki mbunge tu wa Kongwa kwa mara nyingine. Habari ya kuwania uspika sina kabisa, wala huo unaibu spika mimi sitamani chochote ila ndoto zangu ni kuwa mbunge tu.”
Akizungumzia mgongano wa maslahi ya wabunge kuwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kadhalika wajumbe wa bodi mbalimbali za mashirika ya umma, Ndugai anasema hilo si tatizo na iwapo Serikali itaona haifai, basi italiangalia kwa mapana zaidi.
Anasema kuwa ni lazima kuwepo kwa mgawanyo wa madaraka huo ndiyo unaoweza kuwatenganisha na si vinginevyo. “Hilo pia lipo kwa wabunge kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya.


“Kuongelea wabunge kuwa kwenye bodi ni kuwaonea tu, hili ni suala la structure (muundo) wa nchi, kuwe na separation of powers (mgawanyo wa madaraka), kama tunabadilisha mfumo basi tubadili mfumo wote,” anasema Ndugai.
Anaongeza kwa kueleza kuwa mbunge anaweza kufaa katika nafasi ya ujumbe wa bodi kutokana na ujuzi wake alionao, hivyo taasisi husika ikiona anafaa humteua ili awasaidie katika utendaji kazi, hivyo si busara kuwanyooshea vidole kutokana na nafasi hizo.