Na Benny Mwaipaja, JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na Biashara ya Nje wa Sweden, Diana Janse, jijini Dodoma, ambapo Naibu Waziri huyo, amemweleza Dkt. Nchemba kuwa, nchi yake inaandaa Mkakati Mpya wa Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unaolenga kuongeza ushirikiano katika nyanja za kiuchumi na kibiashara.

Katika mazungumzo yao, Dkt. Nchemba aliishukuru Sweden kwa kusaidia maendeleo ya nchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika sekta za nishati, elimu, maendeleo ya jamii kupitia Mfuko wa TASAF pamoja na mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR, kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida ambacho ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 96.

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (wapili kulia), Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na Biashara ya Nje wa Sweden Mhe. Diana Janse (wapili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo  (kulia) na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Ozaki Macias, baada ya kumalizika kwa kikao kilichojadili kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na utekelezaji wa miradi ikiwemo elimu, usawa wa kijinsia, mazingira na masuala ya miundombinu hususan reli ya SGR kilichofanyika jijini Dodom

Aidha, Dkt. Nchemba ameishukuru Sweden kwa kuonesha nia ya kutoa zaidi ya dola za Marekani milioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tatu na cha nne cha reli ya kisasa SGR, fedha ambazo nchi hiyo itazitoa hivi karibuni baada ya kukamilika kwa tathimini ya mazingira ya mradi huo.

Kuhusu Mkakati Mpya wa Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Waziri wa Fedha, Dkt. Nchemba aliahidi kuwa Tanzania itashiriki kikamilifu katika kufanikisha mkakati huo na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Sweden kuja kuwekeza mitaji na teknolojia hapa nchini ili kuchochea akuaji wa uchumi, ajira na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Naibu Waziri huyo wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Diana Jense, alisema kuwa nchi yake inatambua kuwa mradi wa Reli ya Kisasa ni moja ya miradi ya kipaumbele kwa Tanzania na kwamba nchi yake iko tayari kushiriki katika ujenzi wa mradi huo.

Alisema pia kuwa mwelekeo mpya wa ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Sweden utajielekeza zaidi katika masuala ya kiuchumi na kibiashara ambapo utalenga zaidi kuvutia uwekezaji kupitia sekta binafsi.

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akimkabidhi zawadi Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na Biashara ya Nje wa Sweden Mhe. Diana Janse, baada ya kumaliza kikao kilichojadili kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na utekelezaji wa miradi ikiwemo elimu, usawa wa kijinsia, mazingira na masuala ya miundombinu hususan reli ya SGR kilichofanyika jijini Dodoma.

Aidha, katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Balozi wa Sweden Nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias na naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Chriastian Omolo, Viongozi hao walijadili kuhusu uwekezaji katika mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam ambapo nchi hiyo inataka kuwekeza kupitia kampuni ya Scania, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya usafiri katika jiji hilo la kibiashara.

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (watano kulia) na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na Biashara ya Nje wa Sweden Mhe. Diana Janse (wanne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa kikao kilichojadili ushirikiano na utekelezaji wa miradi ikiwemo miundombinu ya reli SGR kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo (wanne kulia),  Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Ozaki Macias (wa pili kushoto) na baadhi ya Makamishna wa Wizara ya Fedha na watumishi wa Ofisi ya Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania kilichofanyika jijini Dodoma.
aziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na Biashara ya Nje wa Sweden Mhe. Diana Janse (hawapo pichani) kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha , Bi. Jenifa Christian Omolo, Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Ozaki Macias na baadhi ya Makamishna wa Wizara ya Fedha na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania, kilichofanyika jijini Dodoma.

By Jamhuri