Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Simon Mayeka amezielekeza Taasisi za Umma Wilayani Kongwa kuwa na mipango ya muda mrefu ya matumizi ya ardhi, itakayowezesha uhifadhi wa mazingira.

Aidha amewataka wananchi kushiriki kwenye shughuli za utunzaji wa mazingira kwa kufanya usafi wa kila jumamosi na upandaji miti katika maeneo yao.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Januari 16, 2024 Mayeka amesema Kampeni ya usafi wa kila jumamosi inapaswa kutiliwa mkazo na kwamba Wananchi waliopakana na barabara wanawajibika kusafisha hadi barabarani bila kuweka mipaka.

“Katika siku za usafi wa Mazingira wafanya biashara hawana sababu ya kufunga maeneo yao ya biashara kwani kinachotakiwa ni kuhakikisha mazingira yanayowazunguka yanakuwa katika hali ya usafi,” Mayeka.

Mayeka pia ametoa wito kwa jamii na taasisi za umma kuachana na mazoea ya kupanda miti mingi kwa pamoja pasi na mikakati thabiti ya kuitunza huku akipiga marufuku ukataji holela wa miti pasipokuwa na vibali.

” Vibali vya kukata miti vinatolewa na Ofisi ya mkuu wa Wilaya au kwa Watendaji wa kata kwa niaba,Taasisi zote za umma zinapaswa kutekeleza agizo la upandaji miti kama ilivyoazimiwa ili wananchi waweze kuhamasika na kuunga mkono jitihada za serikali katika uhifadhi wa mazingira, “amesisitiza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo amesema Halmashauri imekusudia kupanda miti kwenye eneo lote la Hospitali ya Wilaya lenye ukubwa wa ekari 21, kwa kuwa ipo miche ya kutosha ambapo zaidi ya miti 200 imepandwa katika hafla hiyo.

Kwa upande wake Afisa Maliasili na mazingira wa Wilaya hiyo Godfrey Mujairi ametaja shughuli za kibinadamu kuwa zinaleta athari kwenye mazingira ikiwemo uvamizi wa misitu na maeneo ya uchimbaji madini, ukataji miti ovyo, kilimo na ufugaji holela na utupaji hovyo taka kando ya barabara.

By Jamhuri