Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania na India zimekubaliana kuinua uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili hadi kiwango cha Ushirikiano wa Mkakati.

Rais Samia ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini India ambapo amesema dhamira ya Serikali ni kuimarisha na kukuza urafiki na ushirikiano wa nchi mbili, ambao umekuwepo kwa miongo kadhaa.

Rais Samia amesema mazungumzo “yaliyofanyika kwa uwazi na kwa urafiki” na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Narendra Modi wa India, yalisisitiza nia na dhamira ya pande zote mbili za kuimarisha na kuongeza uhusiano wa nchi mbili kwa viwango vikubwa zaidi.

“Tumeafikiana kufungua njia mpya za ushirikiano pamoja na kuongeza ushirikiano wetu hadi kufikia mfumo wa ushirikiano wa Mkakati,” Samia amesema katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Modi katika mji mkuu wa India, baada ya mazungumzo ya pande mbili.

Ameelezea India kuwa “kama mwanafamilia wa karibu,” Rais Samia alifurahishwa na ukweli kwamba biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili unaendelea kuongezeka.

“Hadi mwaka 2022, takwimu zetu za biashara (kati ya pande mbili) zilifikia dola bilioni 3.1. Hivyo, hii inafanya India kuwa mshirika wa tatu kwa biashara nchini Tanzania na mwekezaji wa tano kwa ukubwa nchini,” amesema.

Rais amekaribisha uamuzi wa Taasisi ya Teknolojia ya India (IT) kufungua tawi lake la kwanza nje ya nchi huko Tanzania.

kiongozi huyo amesema Tanzania na India pia wanashirikiana katika maeneo mengine kadhaa, ikiwa ni pamoja na maji safi na salama, ulinzi na usalama.

Rais Samia amempongeza Modi kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa G20 huko New Delhi mwezi uliopita ambapo Waziri Mkuu wa India alipigania kwa mafanikio uanachama kamili wa Afrika katika G20, misamaha ya madeni kwa nchi dhaifu, mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, taasisi za fedha za kimataifa, na Shirika la Biashara Ulimwenguni.