Na Scola Malinga, WF, Dar es Salaam

Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran zimesani makubaliano ya majadiliano ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili baada ya kufanyika kwa majadiliano ya kina kati ya nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yamesaniwa Jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera na Utafiti, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, kwa upande wa Tanzania na Mkurugenzi wa Sheria na Mikataba ya Kodi wa Irani, Dkt. Hossein Abdollah

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Bw. Mhoja alisema kuwa makubaliano hayo yanahusu misingi ya utozaji kodi ya mapato katika shughuli zinazofanywa na raia, kampuni na taasisi za nchi mojawapo kwenye nchi hizo.

“Makubaliano hayo yanaweka misingi ya ushirikiano katika usimamizi wa kodi kati ya mamlaka za usimamizi wa kodi za nchi hizi mbili kupitia ubadilishanaji wa taarifa za kikodi na kusaidiana kwenye masuala ya kodi”, alisema Bw. Mhoja

Alisema kuwa kusainiwa kwa makubaliano hayo kulianza na majadiliano yaliyofanyika kuanzia tarehe 15 hadi 18 Januari 2024, jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa yalikuwa ya duru ya tatu kutokana na kushindwa kufikia maridhiano katika duru mbili zilizotangulia.

Bw. Mhoja alieleza kuwa, Tanzania na Iran zina ushirikiano wa kihistoria katika masuala mbalimbli ya kiuchumi hivyo kukamilika kwa majadiliano na kusainiwa kwa makubaliano hayo kutaimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa kufungua fursa mpya za ajira, biashara na uwekezaji.

Kufuatia kukamilika kwa majadiliano hayo, inasubiriwa kukamilika kwa taratibu za ndani za kisheria kwa kila nchi kuwezesha Mkataba kuridhiwa na kusainiwa ili kuanza kutekelezwa.

Majadiliano hayo yameshuhudiwa na Balozi wa Iran nchini Tanzania Mhe. Hossein Alvandi Behine na Mkurugenzi wa Idara ya Nchi za Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima.

Aidha wajumbe wa pande zote mbili wamezipongeza Timu za Wataalam kutoka nchi hizo kwa kuendesha majadiliano hayo kwa weledi na kuzingatia maslahi ya kila nchi na hatimaye kuweza kufikia maridhiano.

Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera na Utafiti, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja na Mkurugenzi wa Sheria na Mikataba ya Kodi wa Irani, Dkt. Hossein Abdollah, wakisaini mkataba wa makubaliano ya majadiliano ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili baada ya kufanyika kwa majadiliano ya kina kati ya nchi hizo mbili, jijini Dar es Salaam.

Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera na Utafiti, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja na Mkurugenzi wa Sheria na Mikataba ya Kodi wa Irani, Dkt. Hossein Abdollah, wakibadilishana mkataba wa makubaliano ya majadiliano ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili baada ya kufanyika kwa majadiliano ya kina kati ya nchi hizo mbili, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Idara ya Nchi za Mashariki ya Kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima na Balozi wa Iran nchini Tanzania Mhe. Hossein Alvandi Behine wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya majadiliano ya kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili kati ya nchi hizo mbili, jijini Dar es Salaam.

Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera na Utafiti, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja na Mkurugenzi wa Sheria na Mikataba ya Kodi wa Irani, Dkt. Hossein Abdollah, wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa pande hizo mbili baada ya kusainiwa makubaliano ya majadiliano ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili kati ya nchi hizo mbili, jijini Dar es Salaam.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

By Jamhuri