Na Allan Vicent, JamhuriMedia,Tabora

TANZANIA inatarajiwa kuungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya mbolea duniani itakayofanyika Kitaifa Mkoani Tabora kuanzia tarehe 11 hadi 13 Oktoba mwaka huu katika Uwanja wa Chipukizi uliopo katika Halmashauri ya Manispaa Tabora.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dk Batilda Burian amesema maadhimisho hayo ni muhimu sana kwa kuwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali.

Alibainisha kuwa maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali za wakulima ikiwemo pembejeo (mbolea, mbegu na viuatilifu) zitakazooneshwa na makampuni yanayouza pembejeo hapa nchini.

RC Batilda aliongeza kuwa kampuni zaidi ya 15 zinazojihusisha na uagizaji na uuzaji mbolea nchini, Mashirika na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo na Taasisi za fedha ni miongoni mwa wadau watakaoshiriki maonesho hayo.

Alisema kupitia maadhimisho hayo wataalamu kutoka taasisi za utafiti, kampuni za mbolea, vyuo vikuu, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa kilimo watapata fursa ya kutoa elimu sahihi ya matumizi ya mbolea kwa wakulima.

Aidha watatoa elimu ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu, afya ya udongo, matumizi ya mbegu bora na udhibiti wa tasnia ya mbolea.

Alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni Agenda 10/30: Matumizi Sahihi ya Mbolea ya Ruzuku kwa Kilimo chenye Tija kauli ambayo imebeba ujumbe wenye matumaini mapana kwa wakulima.

‘Tunamkushukuru sana Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga sh bil 150 kwa mwaka wa fedha 2022/23 ili kugawa ruzuku ya mbolea kwa wakulima lengo likiwa kuwapunguzia makali’, alisema.

RC aliongeza kuwa kupitia rukuzu hiyo Mkoa ulipokea na kutumia zaidi ya tani 8,000 za mbolea zenye thamani ya sh bil 8.5 kwa mwaka jana ambapo jumla ya wakulima 29,517 walinufaika na mbolea hiyo.

Alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa mbolea ya ruzuku ili kuinua wakulima wote nchini na hata msimu huu pia ametenga zaidi ya sh bil 150 kwa ajili ya kutekeleza mpango huo.

Dkt Batilda alibainisha kuwa Mkoa umepanga kuongeza vituo vya kuuzia mbolea kutoka 27 vya sasa hadi 80 ili kumaliza changamoto ya wakulima kutembea umbali mrefu na kuwataka kwenda kujiandikisha katika Ofisi za Vijiji na Mitaa.

Alitoa wito kwa wakulima na wadau wote wa sekta ya kilimo kuja katika maadhimisho hayo ili kujifunza teknolojia mbalimbali za matumizi sahihi ya mbolea, afya ya udongo, viuatilifu na mbegu bora ili kupata mafanikio makubwa.

By Jamhuri