Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Tabora

Waziri wa Ujenzi Profesa Makame Mbarawa amemwagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Makutupora-Tabora kuongeza kasi ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Ametoa agizo hilo jana baada ya kutembelea eneo la mradi kuanzia Makutupora (Dodoma) hadi Tabora ili kujionea maendeleo ya mradi ambapo ameonesha kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi, kampuni ya Yapi Merkezi.

Amesema kasi ya ujenzi wa kipande hicho chenye urefu wa km 294 na km 74 za kupishana hairidhishi, akatoa mfano wa ujenzi wa tuta la reli hiyo ambalo limechukua muda mrefu sana, hivyo akamwagiza kuongeza kasi ili kufidia muda uliopotea.

Waziri Mbarawa alisema Mkandarasi alipaswa kuwa amefikia takribani asilimia 22 ya mradi huo hadi sasa, lakini cha kusikitisha amefikia asilimia 12 tu, hili halikubaliki, anafanya kazi nzuri na yenye viwango lakini kasi yake imepungua.

Alimtaka kufanya kila linalowezekana ili kufidia muda uliopotea na kuelekeza Mkandarasi Mshauri Kampuni ya Korea Rail kumsimamia ipasavyo ili kazi hiyo itekelezwe kwa viwango na kwa wakati kama mkataba unavyotaka.

‘Spidi tuliyotegemea sio hii anayokwenda nayo sasa, anafanya kazi nzuri ndiyo, lakini bado anasuasua, nataka aje na mpango kazi wa kufidia muda uliopotea ili mradi huu ukamilike haraka’, amesema.

Amebainisha kuwa mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya dola za Kimarekani bilioni 1.908 sawa na sh trilioni 4.408 unaendelea vizuri lakini changamoto kubwa iliyopo ni kusuasua kwake.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRL) Mhandisi Senzige Kisenge alisema mradi huu ulioanza kutekelezwa mwaka jana unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2026.

Amesisitiza kuwa tayari wamemwelekeza Mkandarasi kuandaa mpango kazi utakaomwezesha kutekeleza mradi huo kwa kasi na viwango na kwa wakati ikiwemo kufidia muda uliopotea.

By Jamhuri